Guterres atoa wito wa ulimwengu ambako "hakuna mtu anayeuzwa au kununuliwa"
-
António Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito wa kuwepo ulimwengu "ambapo hakuna mtu anayenunuliwa, kuuzwa au kunyonywa," akisisitiza udharura wa kuchukuliwa hatua za pamoja za kusaidia waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu na kuwawajibisha wahalifu.
Guterres amesema katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Biashara Haramu ya Binadamu, kuwa biashara haramu ya binadamu ni uhalifu wa kutisha na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Ameongeza kuwa uhalifu huu unawakilisha mojawapo ya "aina za uhalifu uliopangwa unaokua kwa kasi zaidi, unaoendeshwa na mitandao isiyo na huruma ambayo hutumia mazingira magumu na kufaidika kutokana na maumivu ya watu."
Guterres ameitaja biashara ya binadamu kuwa "shughuli ya kikatili ya kupangwa na inayofanyika kwa msingi wa udanganyifu, kulazimishwa na unyonyaji, na inayokuwa kwa kasi," akisisitiza kwamba vikundi vya uhalifu "vinafanya kazi kuvuka mipaka kwa kasi na njia tata za kutisha."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuwepo umoja na hatua za haraka katika kupambana na biashara haramu ya binadamu.
Guterres amesisitiza haja ya kujenga ushirikiano imara na mashirika ya kiraia na sekta ya kibinafsi, ikiwa ni pamoja na makampuni ya teknolojia, ili kuongeza ufahamu na kuimarisha njia za kuripoti uhalifu huo ili kuzuia unyonyaji na kulinda watu walio katika hatari.
Kwa upande wake, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na zilizoratibiwa kushughulikia mojawapo ya aina za biashara haramu ya binadamu iliyopuuzwa ambayo ni kulazimishwa kutenda uhalifu.
IOM imesema vikundi vya uhalifu hulazimisha watu walio hatarini, wakiwemo wahamiaji, watoto na vijana, kufanya uhalifu kwa kutumia udanganyifu, vitisho na ukatili.