Waziri mkuu wa Australia apuuza shutuma za Netanyahu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129772-waziri_mkuu_wa_australia_apuuza_shutuma_za_netanyahu
Waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese leo amepuuza shutuma za Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya uamuzi wa nchi hiiyo wa kulitambua taifa la Palestina, na kusema anawaheshimu viongozi wa nchi nyingine.
(last modified 2025-08-20T08:45:14+00:00 )
Aug 20, 2025 08:45 UTC
  • Waziri mkuu wa Australia apuuza shutuma za Netanyahu

Waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese leo amepuuza shutuma za Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya uamuzi wa nchi hiiyo wa kulitambua taifa la Palestina, na kusema anawaheshimu viongozi wa nchi nyingine.

Awali Waziri Mkuu wa ghasibu wa Israel alimshutumu mwenzake wa Australia kwa "kuisaliti Israel" na "kutelekeza" jamii ya Wayahudi wa Australia, baada ya siku za mzozo unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.

Benjamin Netanyahu alisema Jumanne kwamba historia itamkumbuka Anthony Albanese "kwa kile alichosema: mwanasiasa dhaifu".

Australia ilimzuia mwanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia wa muungano unaotawala wa Netanyahu kuingia nchini humo siku ya Jumatatu, na Israel nayo ikabatilisha viza za wawakilishi wa Australia kwa Mamlaka ya Palestina.

Waziri wa Uhamiaji wa Australia Tony Burke alisema Netanyahu "ameikosoa" Canberra hivi karibuni baada ya kutangaza kuwa itaungana na Uingereza, Ufaransa na Canada katika kutambua taifa la Palestina.

"Nguvu hazipimwi kwa ni watu wangapi unaoweza kulipua au ni watu wangapi unaweza kuwaacha wakiwa na njaa," Burke aliambia Shirika la Utangazaji la Australia Jumatano.

Serikali ya Australia hivi karibuni ilitangaza kuwa, inatarajia kuitambua rasmi Palestina mwezi ujao wa Septemba.

Waziri Mkuu wa Australia alitangaza kuwa, Canberra italitambua taifa la Palestina kwenye mkutano ujao wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Septemba. "Canberra itatambua haki ya watu wa Palestina kuwa na nchi yao wenyewe," Anthony Albanese aliwaambia waandishi wa habari, kulingana na tovuti ya gazeti la Ufaransa la Le Figaro.