58% ya Wamarekani wanaunga mkono kulitambua taifa la Palestina
Asilimia 58 ya Wamarekani wanaunga mkono hatua ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinazolitambua rasmi taifa la Palestina. Hii ni kwa mujibu wa uchunguzi mpya ya maoni ulioandamana na matumaini kuwa Israel na Hamas zinaweza kufikia makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.
Karibu 33% ya walioshiriki katika uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na Reuters-Ipsos, wamepinga wazo la wanachama wa UN kutambua taifa la Palestina, wakati 9% hawakujibu.
Asilimia 65 ya washiriki katika utafiti huo wamesema Marekani inapaswa kuchukua hatua huko Gaza kusaidia raia wanaosumbuliwa na njaa, huku asilimia 28 wakipinga. Warepublican kutoka chama cha Rais Donald Trump wameunda asilimia 41 ya wale waliopinga.
Uchunguzi huo wa maoni wa siku sita, uliohitimishwa Jumatatu iliyopita, umeonyesha kuwa 59% ya Wamarekani wanaamini kuwa majibu ya jeshi la Israeli huko Gaza yalitiwa chumvi, wakati 33% hawakukubali.
Katika kipindi cha uchunguzi huo wa maoni, washirika watatu wa Marekani—Canada, Uingereza, na Ufaransa—walitangaza nia yao ya kulitambua Taifa la Palestina, na hivyo kuongeza mashinikizo kwa Israel huku njaa ikiendelea kuchukua roho za Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Uingereza, Canada, Australia, na baadhi ya washirika wao wa Ulaya walisema wiki iliyopita kwamba maafa ya binadamu katika eneo lililokumbwa na vita la Palestina umefikia "kiwango kisichoweza kufikirika," huku mashirika ya misaada yakionya kwamba, watu wa Gaza wanasumbuliwa na baa la njaa.