Norway yalaani jinai za Israel Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129994-norway_yalaani_jinai_za_israel_ukanda_wa_gaza
Norway imeutaja ukatili unaofanya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, na kutangaza kwamba nchi hiyo ya Ulaya inafikiria kupiga marufuku makampuni ya Norway kushiriki katika shughuli zinazounga mkono upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2025-08-26T02:47:58+00:00 )
Aug 26, 2025 02:47 UTC
  • Norway yalaani jinai za Israel Ukanda wa Gaza

Norway imeutaja ukatili unaofanya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, na kutangaza kwamba nchi hiyo ya Ulaya inafikiria kupiga marufuku makampuni ya Norway kushiriki katika shughuli zinazounga mkono upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Andreas Motzfeldt Kravik, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway amekosoa hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea katika Ukanda wa Gaza, na kuzitaja hujuma zinazofanywa dhidi ya wakazi wa eneo hilo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway amesisitiza kuwa matukio ya Oktoba 7,2023 hayawezi kuhalalisha vitendo vya jinai vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza ulio chini ya mzingiro. 

Kravik ameukosoa utawala wa Kizyauni kwa kuanzisha vita dhidi ya Wapalestina wa Gaza; vita ambavyo havina uhalali wowote wa kisheria kwa kujibu wa sheria za kimataifa. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway ameongeza kusema: Nchi hiyo imewawekea vikwazo maafisa wa Israel hasa Itamar Ben-Gvir Waziri wa usalama wa Taifa na Bezalel Smotrich Waziri wa Fedha wa utawala huo. 

Kravik ametoa wito wa kuwepo muungano endelevu wa kidiplomasia dhidi ya sera haribifu za utawala ghasibu wa Israel, akikemea matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Sa'ar, aliyependekeza kuwa Ulaya lazima ichague kati ya kuiunga mkono Israel au Hamas.