UN, OIC, EU, RSF na hata waitifaki wa Israel walaani shambulio la kinyama lililoua wanahabari Ghaza
Taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Umoja wa Ulaya, Shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF) na hata nchi kadhaa za Magharibi waitifaki wa utawala wa kizayuni wa Israel zimelaani vikali shambulio la kinyama lililofanywa na jeshi la utawala huo katika Hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis katika Ukanda wa Ghaza.
Olga Cherevko, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ameyaelezea mashambulio yanayofanywa na utawala wa kizayuni kuwa ni ya "kutisha".
Amesema kuona picha za shambulio hilo kwenye televisheni “hakukubaliki,” akiashiria mashambulio mengine ya awali yaliyofanywa na Israel dhidi ya hospitali.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema “kuuawa wanahabari Ghaza inapasa kuuudhi ulimwengu” na kuibua ombi la haki badala ya ukimya.
Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi hiyo, amesema katika taarifa ya maandishi kuwa vifo vya wanahabari katika eneo hilo vinaonyesha umuhimu wa haraka wa kuwajibishwa.
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa, Francesca Albanese, yeye ameyataka mataifa kuchukua hatua za haraka kuzuia “kufurika kwa damu” huko Ghaza.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani mauaji ya wanahabari na wafanyakazi wa vyombo vya habari yaliyofanywa na Israel huko Ghaza na kuyaelezea kuwa ni “uovu wa kivita” na “shambulio dhidi ya uhuru wa waandishi wa habari.”
Shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF) limelaani vikali mashambulio ya Israel, likitaka hatua za haraka zichukuliwe na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia mauaji ya aina hiyo.
Shirika hilo la habari la kimataifa limesema wanahabari watano wa Palestina walilengwa “kwa makusudi” na jeshi la Israel.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen yeye ameitaka Israel iache kuua watu “wanaojaribu kuambia dunia kinachoendelea Ghaza.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uhispania imetoa taarifa ikisema, “Serikali ya Uhispania inalaani shambulio la Israel dhidi ya Hospitali ya Nasser Ghaza, ambalo limesababisha vifo vya wanahabari wanne na raia wasio na hatia”.
Mbali na Uhispania, hata madola mengine ya Magharibi waungaji mkono wakuu wa utawala wa kizayuni ikiwemo Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italia nazo pia zimetoa kauli za kukosoa unyama uliofanywa na utawala huo ghasibu.
Mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Ghaza zimeripoti kuwa, Wapalestina wasiopungua 20, wakiwemo wanahabari watano na mtu mmoja wa kikosi cha Zimamoto, waliuawa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa jana Jumatatu katika shambulio la kinyama lililofanywa na jeshi la kizayuni dhidi ya hospitali ya Nasser iliyoko Khan Younis.
Kwa mujibu wa Mamlaka za Ghaza jeshi la Israel lilipiga makombora mara mbili ghorofa ya nne ya jengo la hospitali, huku shambulio la pili likitokea wakati timu za uokoaji zilipofika kuwahifadhi majeruhi na kuondoa maiti.
Katika shambulio jingine dhidi ya wanahabari, mwandishi wa habari wa Palestina Hassan Douhan aliuawa na jeshi la kizayuni huko Khan Younis, na kufikisha idadi ya wanahabari waliouawa jana Jumatatu kuwa sita.../