Zaidi ya mabalozi 206 wa zamani wa EU wataka Israel ichukuliwe hatua kali
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130034-zaidi_ya_mabalozi_206_wa_zamani_wa_eu_wataka_israel_ichukuliwe_hatua_kali
Zaidi ya mabalozi 200 wa zamani wa Umoja wa Ulaya na maafisa wa ngazi ya juu jana Jumanne waliituhumu Brussels kwa kushindwa kuchukua hatua za kukabiliana na hali mbaya ya binadamu katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.
(last modified 2025-10-16T03:06:03+00:00 )
Aug 27, 2025 02:28 UTC
  • Zaidi ya mabalozi 206 wa zamani wa EU wataka Israel ichukuliwe hatua kali

Zaidi ya mabalozi 200 wa zamani wa Umoja wa Ulaya na maafisa wa ngazi ya juu jana Jumanne waliituhumu Brussels kwa kushindwa kuchukua hatua za kukabiliana na hali mbaya ya binadamu katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Mabalozi hao wa zamani wa EU wamesaini waraka wa pamoja unaoutaka umoja huo kuzidisha mashinikizo kwa Israel ili usitishe vita vya mauaji yake ya kimbari na ukaliaji mabavu dhidi ya eneo hilo. 

Mabalozi hao na maafisa wa ngazi ya juu wa zamani wa EU wamesema katika waraka wao huo wa pamoja kwamba: Wanaeleza masikitiko yao makubwa kuhusu kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo katika Uknda wa Gaza na kwamba Umoja wa Ulaya hadi sasa haujachukua hatua zozote muhimu za kuishinikiza Israel isitishe vita vyake vya ukatili, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo, na kuondoa mzingiro wake haramu dhidi ya watu wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Mabalozi hao wa zamani wa Umoja wa Ulaya pia wametahadharisha kuwa iwapo umoja huo utashindwa kuchukua msimamo chanya basi nchi wanachama au makundi ya nchi zenye misimamo na nia moja yatapasa kuchukua hatua katika uwanja huo. 

Waraka huo wa mabalozi na maafisa wa ngazi ya juu wa zamani wa Umoja wa Ulaya pia umelaani mipango ya serikali ya Israel ya kupanua ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Quds Mashariki. Waraka huo umeitaja mipango hiyo ya utawala wa kizayuni kuwa njama za wazi za Israel za kuhujumu suluhisho la muda mrefu la serikali mbili linaloungwa mkono na aghalabu ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na EU.