Venezuela yapeleka meli za kivita, ndege zisizo na rubani pwani, wakati kikosi cha wanamaji cha Marekani kikikaribia
Venezuela imetangaza kuwa imepeleka meli za kivita na ndege zisizo na rubani kwenye eneo lake la maji na kufanya doria kwenye ufuo wa pwani ya nchi hiyo ili kukabiliana na hatua ya Marekani ya kutuma meli kadhaa za kivita katika eneo la Karibea kwa kile ilichodai ni kwa ajili ya kukabiliana na biashara ya madawa ya kulevya na kumshinikiza Rais Nicolás Maduro.
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino, amesema katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba "doria za majini zimetumwa kwenye Ghuba ya Venezuela na pwani ya Karibea, na meli kubwa kaskazini mwa eneo letu la maji," pamoja na "idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani."

Maafisa wakuu wa Venezuela wamethibitisha kuwa nchi yao itakabiliana na kile walichokitaja "uchokozi" wa Marekani. Rais Nicolás Maduro wa Venezuela ametangaza kuanzishwa "mpango maalumu wenye zaidi ya watu milioni 4.5 wenye silaha," akilaani jaribio la Marekani la kutaka "kubadilisha utawala" katika nchi yake na "shambulio la kigaidi la kijeshi."
Wiki iliyopita, Washington ilitangaza kuwa imetuma meli tatu za kivita za kurusha makombora katika eneo la karibu na Venezuela. Siku ya Jumanne, afisa mmoja wa Marekani, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa sambamba na meli hizo za kivita, Washington imetuma meli yenye makombora ya kuongozwa na manowari ya nyuklia ya kushambulia kwa kasi.
Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani pia vimeripoti kwamba Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) inakusudia kutuma wanajeshi 4,000 wa majini kwenye eneo la Karibea karibu na pwani ya Venezuela.
Caracas inazitazama hatua hizi za Marekani kama harakati za "kuongezeka kwa uhasama," na Jumanne iliyopita iiliwasilisha ombi kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati mzozo huo, na "kusitishwa mara moja kutumwa wanajeshi wa Marekani katika visiwa vya Caribbean."
Caracas na Washington zimekuwa katika msuguano kwa miaka mingi, na Rais wa Marekani Donald Trump amezidisha mashinikizo kwa mwenzake wa Venezuela, Nicolás Maduro, ambaye nchi yake inapinga vikali sera za kijuba na kibeberu za Marekani.