Aliyeua watoto kwa bunduki katika skuli ya kanisa Marekani ni mwanamume aliyebadilisha jinsia
Mshambuliaji aliyefyatulia risasi kanisa katika skuli ya kikatoliki kusini mwa mji wa Minneapolis nchini Marekani jana Jumatano na kuua na kujeruhi watu kadhaa ametambuliwa na gazeti la The New York Post kama Robin Westman. Kwa mujibu wa gazeti hilo, inasemekana Westman alibadilisha jina lake la Robert na kuwa Robin mwaka 2020 na kujitambulisha kama mwanamke.
The New York Post limesema, polisi sasa wanachunguza kama manifesto ya dakika 20 iliyowekwa kwenye tovuti ya YouTube saa chache kabla ya kutokea shambulio hilo ina uhusiano na Westman au la. Video hiyo tayari imefutwa kwenye tovuti hiyo.
Katika video hiyo, unaonekana mkono ukigeuza polepole kurasa za daftari jekundu, ambalo limewekwa juu ya kile kinachoonekana kuwa michoro ya bunduki. Pia inaonyesha silaha kadhaa, ikiwa ni pamoja na bunduki ya nusu-otomatiki na bunduki ndogo. Chemba za risasi zinaweza kuonekana pia zikiwa zimeandikwa juu yake "kwa ajili ya watoto," "ua Donald Trump".
Watoto wawili wa umri wa miaka minane na 10 waliuawa na watu 17 walijeruhiwa wakati mshambuliaji huyo alipowafyatulia risasi watoto wa skuli waliokuwa wakihudhuria misa katika skuli hiyo ya kikatoliki ya Annunciation na kisha kujiua yeye mwenyewe.
Mkuu wa Polisi ya Minneapolis, Minnesota, amesema kati ya waliojeruhiwa katika shambulio la Jumatano asubuhi, 14 ni watoto na wawili kati yao hali zao ni mahatuti. Watoto wengine wanaotibiwa wanatarajiwa kupona majeraha yao.../