Malaysia yataka utawala wa kizayuni wa Israel utimuliwe uanachama Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130180-malaysia_yataka_utawala_wa_kizayuni_wa_israel_utimuliwe_uanachama_umoja_wa_mataifa
Malaysia imetoa mwito wa kusimamishwa uanachama wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa kutokana na jinai zake katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-08-30T03:54:03+00:00 )
Aug 30, 2025 03:54 UTC
  • Malaysia yataka utawala wa kizayuni wa Israel utimuliwe uanachama Umoja wa Mataifa

Malaysia imetoa mwito wa kusimamishwa uanachama wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa kutokana na jinai zake katika Ukanda wa Gaza.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Malaysia Mohamad Hassan ambaye amesisitiza kuwa, kuna haja ya kusimamisha uanachama wa utawala wa kizayuni katika Umoja wa Mataifa na kuwekewa vikwazo vikali, akitolea mfano vita vinavyoendelea vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Takwa la Malaysia linaonyesha hali ya masikitiko inayoongezeka Kusini mwa Ulimwengu kutokana na kutochukuliwa hatua za kimataifa dhidi ya ukatili wa utawala wa Kizayuni. Mwito huo wa Malaysia unaweza kuhimiza mataifa yenye Waislamu wengi zaidi na yasiyofungamana na upande wowote kufuata hatua kama hizo, na kuitenga zaidi Tel Aviv kidiplomasia.

"Sasa ni wakati wa kusimamishwa uanachama wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Umoja wa Mataifa na vikwazo kuwekwa na nchi zote. Vikwazo vinaweza kupunguza mtiririko wa silaha kwa utawala huu," Hassan alisema, akisisitiza kwamba "sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa inataka kuzuia utekelezaji wa mipango ya utawala wa Kizayuni wa kuikalia na kuiharibu Gaza."

Wakati huo huo, Bunge la Uturuki limetoa taarifa likitaka kusimamishwa uanachama wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa na mashirika yote ya kimataifa hadi jinai za utawala huo katika Ukanda wa Gaza zitakapokoma.

Kwa mujibu wa ripoti hii, Ofisi ya Rais wa Bunge la Uturuki imeyataka mabunge yote duniani kusitisha uhusiano wao wa kijeshi na kibiashara na Israel na kuchukua hatua ya kuvunja mzingiro wa Palestina.