Erdogan: Marekani ichague ima Fathullah Gulen au Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i13063-erdogan_marekani_ichague_ima_fathullah_gulen_au_uturuki
Katika kile kinachoonekana kuendelea kuingia doa uhusiano kati ya Ankara na Washington, Rais wa Uturuki ametoa machaguo mawili kwa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 11, 2016 08:57 UTC
  • Erdogan: Marekani ichague ima Fathullah Gulen au Uturuki

Katika kile kinachoonekana kuendelea kuingia doa uhusiano kati ya Ankara na Washington, Rais wa Uturuki ametoa machaguo mawili kwa Marekani.

Rais Recep Teyyip Erdogan amesema kuwa Ankara itasitisha ushirikiano wake wa kistratejia na Washington iwapo Marekani itaendelea kumpa hifadhi Fathullah Gulen, shakhsia wa kidini anayeipinga serikali ya Uturuki  ambaye yuko uhamishoni nchini Marekani. Akizungumza katika Ikulu ya Rais mjini Ankara, Rais Erdogan amesema Marekani haina budi kuchagua ima kuendelea kuwa na uhusiano mzuri na Uturuki au iendelee kumpa hifadhi shakhsia huyo wa kidini ambaye Uturuki inamtuhumu kuwa gaidi mwenye misimamo ya kuchupa mipaka.

Fathullah Gulen, shakhsia wa kidini aliyepewa hifadhi na Marekani

Rais  Recep Teyyip Erdogan amesema serikali yake imeitumia Marekani mafaili 85 kuthibitisha kuwa Gulen alihusika na jaribio hilo la mapinduzi lililofeli mwezi uliopita. Hata hivyo, Gulen mwenye umri wa miaka 75 amekanusha kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi.

Jaribio la mapinduzi lililofeli Uturuki, Julai 15

Erdogan amekuwa akisisitiza kuwa, jaribio hilo la mapinduzi lilifanywa na nchi za Magharibi na kwamba tukio hilo lisingeweza kuongozwa na kuratibiwa kutoka ndani tu ya nchi. Watu wasiopungua 246 waliuawa huku wengine zaidi ya 2,100 wakijeruhiwa katika jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi la Julai 15.