Umoja wa Mataifa wataka kukomeshwa uvamizi wa Israel dhidi ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133762-umoja_wa_mataifa_wataka_kukomeshwa_uvamizi_wa_israel_dhidi_ya_palestina
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kukomeshwa kuikalia kwa mabavu Palestina na kulaani ukiukwaji mkubwa wa haki za Wapalestina katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
(last modified 2025-11-30T04:10:46+00:00 )
Nov 30, 2025 04:10 UTC
  • Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka kukomeshwa uvamizi wa Israel dhidi ya Palestina
    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ataka kukomeshwa uvamizi wa Israel dhidi ya Palestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kukomeshwa kuikalia kwa mabavu Palestina na kulaani ukiukwaji mkubwa wa haki za Wapalestina katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amsema hayo alipohutubia  kikao maalum mjini New York Marekani kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina na kusisitiza haki ya watu wa Palestina ya kupata utu, uadilifu na kujitawala na kubainisha kwamba, haki hizo zimekiukwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Guterres aidha amesisitiza haki isiyoweza kupokonywa ya wananchi wa Palestina ya kuanzisha taifa lao huru na kutoa wito wa kukomeshwa uvamizi wa mabavu wa ardhi za Palestina, suala ambalo pia limetambuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Akizungumzia uharibifu na uharibifu wa Gaza, mauaji ya makumi ya maelfu ya watu, hasa watoto na wanawake, na ukatili wa walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza umuhimu wa kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na kuunga mkono Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kupigwa hatua kuelekea suluhisho la serikali mbili kulingana na mipaka ya 1967 na kuteuliwa Baytul-Muqaddas kama mji mkuu wa pamoja.

Guterres pia amezungumzia mauaji ya waandishi wa habari, wafanyakazi wa vyombo vya habari, na wafanyakazi wa kibinadamu, akisema kwamba idadi hii imefikia kiwango cha juu zaidi tangu Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.