Ripoti yatahadharisha: Mamilioni ya Waingereza Waislamu wako hatarini kuvuliwa uraia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134296-ripoti_yatahadharisha_mamilioni_ya_waingereza_waislamu_wako_hatarini_kuvuliwa_uraia
Mamlaka ya kunyang'anya uraia yanayoelezewa kuwa ni ya "kupindukia mpaka na yenye usiri" iliyopewa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza yanawaweka mamilioni ya Waislamu raia wa nchi hiyo katika hatari ya kuvuliwa uraia wao.
(last modified 2025-12-14T09:45:19+00:00 )
Dec 14, 2025 09:45 UTC
  • Ripoti yatahadharisha: Mamilioni ya Waingereza Waislamu wako hatarini kuvuliwa uraia

Mamlaka ya kunyang'anya uraia yanayoelezewa kuwa ni ya "kupindukia mpaka na yenye usiri" iliyopewa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza yanawaweka mamilioni ya Waislamu raia wa nchi hiyo katika hatari ya kuvuliwa uraia wao.

Utafiti uliofanywa na taasisi mbili za Runnymede Trust na Reprieve umegundua kuwa watu milioni tisa nchini Uingereza, ikiwa ni takribani asilimia 13 ya idadi ya watu wote wanaweza kuvuliwa uraia wao kisheria kulingana na atakavyoamua tu waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo.

Wanaharakati wametahadharisha kwamba, mamlaka hayo yanaathiri na kuwaweka hatarini kwa kiasi kikubwa raia wenye asili ya Asia Kusini, Mashariki ya Kati na Afrika.

Taasisi zote hizo mbili zimetahadharisha kuwa, "sheria ya unyimaji" sasa inatoa tishio la kimfumo kwa jamii za Waislamu, ikiakisi ubaguzi unaofanywa na serikali dhidi ya raia wa Uingereza wenye uhusiano wa kifamilia na Carribean katika kashfa ya Windrush.

Chini ya sheria ya sasa, raia wa Uingereza wanaweza kupoteza uraia wao ikiwa serikali itaamini kwamba, wanafaa kuwa na uraia wa nchi nyingine, hata kama hawajawahi kuishi katika nchi hiyo au hawajitambulishi nayo.

Ripoti inaonyesha kuwa, watu wenye mfungamano na Pakistan, Bangladesh, Somalia, Nigeria, Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, ambazo zote ni nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaouunda jamii ya Waislamu wa Uingereza, ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini zaidi kukumbwa na fagio la kuvuliwa uraia.

Wanaharakati wanasema, hali hiyo imejenga mfumo wa uraia wa kidaraja kulingana na asili ya mtu, ambapo kuhusishwa Waislamu na Uingereza kunawekewa masharti ambayo hayawekwi kwa Waingereza wazungu.../