Kwa nini Ulaya inataka kufafanua upya uhusiano wake na China?
Ufaransa na nchi nyingine nne za Ulaya, katika mkesha wa mkutano wa kimkakati wa Kamisheni ya Ulaya kuhusu China, zilitoa wito wa kuundwa vyombo vipya vya kutetea biashara ili kulinda viwanda vya Ulaya na kukabiliana na ushindani kutoka kwa makampuni yanayoungwa mkono na serikali ya Beijing.
Katika mtazamo wa awali, habari hii inaonekana kama mzozo wa kibiashara tu kati ya washirika wawili wakubwa wa kiuchumi duniani, lakini kwa hakika ni ishara ya mabadiliko ya kina katika muundo wa uhusiano wa China na Umoja wa Ulaya. Mabadiliko ambayo yanaweza kusababisha mojawapo ya matukio muhimu zaidi ya kijiografia duniani katika muongo ujao.
Ili kuelewa umuhimu wa mabadiliko haya, tunapasa kutazama mbali zaidi kuliko migogoro ya sasa kuhusu ushuru, magari ya umeme au chuma. Kinachotokea Brussels leo kinaonyesha wasiwasi unaoongezeka wa Ulaya kuhusu ushindani wake wa kiviwanda na China. Katika miongo miwili iliyopita, China imegeuka kutoka kituo cha utengenezaji wa bidhaa zenye thamani ya chini na kuwa moja ya nchi zinazoongoza duniani kwa nguvu za kiviwanda na kiteknolojia kwa kutekeleza sera za muda mrefu za viwanda, kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu, kuendeleza teknolojia zinazoinukia na kuunga mkono viwanda vya kimkakati. Viwanda vingi vya Ulaya sasa vinakabiliwa na mshindani mkubwa ambaye ameteka soko la Ulaya kwa gharama ya chini ya uzalishaji bidhaa. Nakisi ya biashara ya Ulaya na Uchina, inakadiriwa kuwa Euro bilioni 360 kufikia mwa uliopita wa 2025, jambo linalochochea wasiwasi huu. Wanasiasa wengi wa Ulaya wanaona makisi hii ya biashara kama ishara ya kutofautiana kimuundo katika mahusiano ya kiuchumi na China.
Kinachoongeza wasiwasi wa Brussels sio tu idadi ya mauzo ya nje ya China, bali ni hali ya mabadiliko ya mauzo haya ya nje. Katika miaka ya nyuma, Ulaya ilikuwa akiagiza bidhaa za bei nafuu kutoka China, lakini sasa sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya China barani Ulaya ni pamoja na magari ya umeme, betri za lithiamu, paneli za jua na teknolojia ya hali ya juu, bidhaa ambazo zilipaswa kuwa injini za ukuaji wa uchumi wa Ulaya katika enzi za mabadiliko ya kijani kibichi. China imebadilika kutoka mshirika wa kibiashara na kuwa mshindani wa moja kwa moja kwa mustakabali wa viwanda wa Ulaya. Ni katika muktadha huu ndipo wito uliotolewa na Ufaransa, Italia, Uhispania, Uholanzi na Lithuania kwa ajili ya kuanzishwa vyombo vipya vya kulinda biashara unapaswa kutathminiwa. Nchi hizi zinaamini kuwa sheria za jadi za biashara huria hazitoshi tena kushindana na uchumi unaopata uungaji mkono mkubwa wa serikali. Kwa hivyo zinadai kwamba Ulaya inapasa kutoza ushuru mpya, kutumia viwango vya uagizaji na kuzilinda sekta zake nyeti, kwa kisingizio cha masuala ya usalama wa kiuchumi na kitaifa.
Mtazamo huu unaonyesha mabadiliko ya Ulaya kutoka kwenye mkondo wa kawaida wa biashara huria hadi ulinzi wa kimkakati, mwelekeo ambao pia umekuwa ukishuhudiwa huko Marekani. Suala hili halionekani tu kwenye ushindani wa kiuchumi. Uzoefu wa vita vya Ukraine na utegemezi wa Ulaya kwa nishati ya Russia umebadilisha kimsingi namna viongozi wa Ulaya wanavyotathmini utegemezi wa kiuchumi. Sasa kuna wasiwasi huko Brussels kwamba kuitegemea sana China katika masuala ya madini adimu, betri, chipu na teknolojia za hali ya juu kunaweza kuwa hatari ya kimkakati katika siku zijazo. Vikwazo vya China vya kuuza nje baadhi ya madini muhimu katika miaka ya hivi karibuni pia vimeongeza wasiwasi huu.
Kuhusu suala hili, sera ya "kupunguza hatari" iliyopendekezwa na Tume ya Ulaya kwa kweli ni jaribio la kupunguza utegemezi nyeti bila kukata kabisa uhusiano wa kiuchumi na China. Katika upande wa pili, China inaziona hatua hizi kama ishara ya kuongezeka juhudi za Ulaya katika kulinda viwanda vyake na kuonya kwamba itachukua hatua za kukabiliana na vikwazo vyovyote vipya. Beijing inaamini kwamba tuhuma nyingi zinazotolewa kuhusu uwezo wa ziada wa uzalishaji bidhaa au ushindani usio halali zinaathiriwa na anga ya kijiografia na ushindani mkubwa wa nguvu, badala ya kuwa na misingi ya kiuchumi. Kwa mtazamo wa China, mauzo ya nje ya magari ya umeme, betri na teknolojia ya kijani ni jibu kwa mahitaji halisi ya soko la kimataifa na haja ya Ulaya ya mpito wa nishati, na kwamba kuzuia mauzo hayo kutaongeza tu gharama kwa watumiaji wa Ulaya.
Hata hivyo, kikwazo muhimu zaidi kinachozuia kubuniwa sera moja ya Ulaya ni mgawanyiko wa ndani barani humo. Ufaransa inataka mbinu kali zichukuliwe, lakini Ujerumani, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, inasalia kuhofia matokeo ya mzozo mkubwa wa kibiashara na China. Makampuni makubwa ya Ujerumani yanapata sehemu kubwa ya mapato yao kutoka kwa soko la Uchina na yana wasiwasi kuwa kuongezeka kwa mvutano kunaweza kuipelekea China kulipiza kisasi dhidi ya nchi za Ulaya. Kutofautiana huku kwa mitazamo kunamaanisha kuwa Umoja wa Ulaya bado haujafikia muafaka kamili wa namna ya kukabiliana na China.
Kwa kifupi, kinachoendelea leo kati ya Brussels na Beijing sio mzozo wa ushuru au nakisi ya biashara. Ulaya inatafakari upya kuhusu siasa za kimsingi zaidi za kiuchumi za miongo mitatu iliyopita, ambazo zinasema kwamba kutegemeana kiuchumi daima huleta utulivu na manufaa ya pande zote husika. Usalama wa kiuchumi, ushindani wa viwanda, na masuala ya kijiografia na siasa ni muhimu kama ilivyo biashara na uwekezaji.
Kwa hiyo mustakbali wa uhusiano wa China na Umoja wa Ulaya si ushirikiano wa wazi kama ilivyokuwa katika siku za nyuma wala vita kamili vya kibiashara. Hali inayowezekana zaidi ni kwamba pande hizi mbili zitaingia katika zama za ushindani unaodhibitiwa, kipindi ambacho ndani yake uchumi utakuwa chombo cha kudhihirisha nguvu na kupata maslahi ya kimkakati, ambapo hatima yake inaweza kuwa na taathira kubwa katika uundaji wa mpangilio mpya wa uchumi wa kimataifa katika miongo ijayo.