Bulgaria yapiga marufuku vazi la burqa kote nchini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i16441-bulgaria_yapiga_marufuku_vazi_la_burqa_kote_nchini
Sasa ni rasmi kuwa Bulgaria imejiunga na baadhi ya nchi za Magharibi zilizopiga marufuku vazi la burqa, baada ya bunge la nchi hiyo kupasisha sheria inayopiga marufuku vazi hilo linalovaliwa na wanawake Waislamu nchini kote.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 01, 2016 04:31 UTC
  • Bulgaria yapiga marufuku vazi la burqa kote nchini

Sasa ni rasmi kuwa Bulgaria imejiunga na baadhi ya nchi za Magharibi zilizopiga marufuku vazi la burqa, baada ya bunge la nchi hiyo kupasisha sheria inayopiga marufuku vazi hilo linalovaliwa na wanawake Waislamu nchini kote.

Chama cha Nationalist Patriotic Front ambacho kinaunga mkono serikali, kiliandaa muswada wa kupigwa marufuku vazi hilo la heshima nchini kote, miezi michache baada ya miji kadhaa ya nchi hiyo kupiga marufuku vazi hilo la staha.

Hatua hiyo imelighadhabisha shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, ambalo limesema kupitia mkurugenzi wake wa bara Ulaya, John Dalhuisen kuwa sheria hiyo ni ya kibaguzi na kandamizi.

Wanawake wa Kiislamu nchini Bulgaria wameghadhabishwa na marufuku ya burqa

Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, Serikali ya Bulgaria ilitangaza kuwa itatoa adhabu na kuwatoza faini ya euro 150 kwa mara ya kwanza na euro 500 kwa mara ya pili kwa wanawake wanaovaa hijabu kamili ya Kiislamu katika maeneo ya umma. Kiasi hicho cha pesa kimetajwa kuwa ni zaidi ya mshahara wa kiwango cha  wastani wa kila mwezi nchini Bulgaria.

Nchi za Magharibi zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na vitu vinavyoonekana kuwa na sura ya Uislamu ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku vazi la burqa. Tayari Canada, Ubelgiji na Ufaransa zimepiga marufuku vazi hilo la stara.