White House: Kuhamishiwa ubalozi wa Marekani Beitul Muqaddas kungali kunachunguzwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24097-white_house_kuhamishiwa_ubalozi_wa_marekani_beitul_muqaddas_kungali_kunachunguzwa
Katika radiamali yake kuhusiana na kuenea habari za kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Beitul Muqaddas katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, ikulu ya White House imesema kuwa suala hilo lingali katika hatua zake za mwanzo na kwamba bado linachunguzwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2017 03:42 UTC
  • White House: Kuhamishiwa ubalozi wa Marekani Beitul Muqaddas kungali kunachunguzwa

Katika radiamali yake kuhusiana na kuenea habari za kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Beitul Muqaddas katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, ikulu ya White House imesema kuwa suala hilo lingali katika hatua zake za mwanzo na kwamba bado linachunguzwa.

Vikivinukuu vyombo vya habari vya Kizayuni, baadhi ya vyombo vya habari vya Kiarabu vilikuwa vimeandika kwamba maafisa wa White House walitazamiwa kutangaza leo Jumatatu kuanza shughuli za kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kuelekea Beitul Muqaddas. Katika kampeni zake za uchaguzi na baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani, Rais Donald Trump wa nchi hiyo alimuahidi Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kwamba serikali ya Washington ingeuhamishia ubalozi wake Beitul Muqaddas mara moja.

Trump akiwa na Netanyahu

Matamshi hayo yalikabiliwa na radiamali kali ya viongozi wa Palestina na wa nchi nyingine duniani. Sheikh Akrama Sabri, hatibu wa Masjidul Aqswa Ijumaa iliyopita alilaani vikali hatua ya kutaka kuhamishiwa ubalozi wa Marekani mjini Beitl Muqaddas na kuongeza kuwa hatua hiyo sio tu kuwa ni kutangaza vita dhidi ya Wapalestina bali pia ni kutangaza vita dhidi ya Waislamu wote duniani. Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya pia hivi karibuni walitahadharisha dhidi ya hatua hiyo ya Marekani ya kutaka kuuhamishia ubalozi wake katika mji mtakatifu wa Beitul Muqaddas.