Nicaragua yakosoa kufumbiwa macho jinai za utawala wa Israel
Serikali ya Nicaragua imekosoa vikali hatua ya kuendelea kukingiwa kifua na kutowajibishwa utawala wa Kizayuni wa Israel licha ya jinai zake za kila uchao dhidi ya Wapalestina.
Denis Moncada, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nicaragua amesema ni jambo lisilokubalika kuendelea kutouwajibisha wala kuuadhibu utawala wa Tel Aviv akisisitiza kuwa, kuna udharura wa kukomeshwa tabia ya Israel kughusubu ardhi za Palestina, kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na kuwadhulumu wananchi wasio na ulinzi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nicaragua ameyasema hayo katika mkutano wa kuiunga mkono Palestina uliofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Managua, chini ya kaulimbiu "Kuunda madaraja pamoja na Wapalestina walioko Amerika ya Kati". Aidha wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Kamati ya Kimataifa ya Kutetea Haki za Wapalestina wameshiriki kwenye mkutano huo, uliofanyika chini ya uenyekiti wa Denis Moncada, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nicaragua.
Nicaragua kwa mara nyingine tena imesisitiza juu ya uungaji mkono wake kwa wananchi wa Palestina na kutoa wito wa kuondolewa mzingiro dhidi ya Gaza.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2010, Nicaragua ilisimamisha uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel kulalamikia kitendo cha utawala huo bandia cha kuushambulia msafara wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi madhulumu wa Palestina wa eneo la Ukanda wa Gaza.