Kiongozi wa chama cha Leba Uingereza: Simamisheni uuzaji silaha kwa Saudia
Kiongozi wa chama cha Leba nchini Uingereza kwa mara nyingine tena ametoa wito wa kusimamishwa uuzaji wa silaha kwa utawala wa Saudi Arabia kutokana na utawala huo kuendeleza mauaji dhidi ya raia wa Yemen.
Jeremy Corbyn, kiongozi wa chama cha Laba nchini Uingereza amesema daima amekuwa akipinga hatua ya Saudi Arabia ya kutumia silaha kuua watu wa Yemen na ametoa wito wa kusitishwa uuzaji wa silaha kwa utawala huo.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uingereza ameongeza kuwa, chama cha Leba kimetangaza waziwazi upinzani wake dhidi ya uvamizi na mashambulizi ya Saudi Arabia huko Yemen na kinataka kurejeshwa amani katika nchi hiyo.
Mwezi Machi mwaka 2015 Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani na nchi nyingine kadhaa zilianzisha mashambulizi makali ya anga, nchi kavu na baharini dhidi ya watu wa Yemen kwa shabaha eti ya kumrejesha madarakani rais aliyejiuzulu na kutoroka nchi wa nchi hiyo, Abdrabbuh Mansur Hadi.
Mashambulizi hayo yameua maelfu ya raia wa Yemen hususan wanawake na watoto wadogo na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International pia limezilaumu nchi zinazouuzia silaha utawala wa Saudi Arabia hususan Uingereza na Marekani ambazo zinatumiwa kuua watu wasio na hatia wa Yemen na kutoa wito wa kukomeshwa mara moja.