Trump akosolewa kwa mahudhurio dhaifu mkutano wa G20, Hamburg
Duru za Marekani zimekosoa mahudhurio dhaifu na mienendo ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo katika mkutano uliomalizika juzi wa viongozi wa nchi za G20 nchini Ujerumani.
Mtandao wa ABC News umeripoti kuwa, Rais Donald Trump ameshusha hadhi ya taifa la Marekani na kuwafanya waitifaki wa Marekani wachanganyikiwe katika mkutano wa G20 mjini Hamburg huko Ujerumani.
Ripoti ya mtandao huo imesema kuwa, Donald Trump ni mtu mbinafsi asiyejali anayosema na kunena.
Ripoti ya ABC News imeongeza kuwa, katika kikao cha G20 huko Hamburg, Marekani ilikuwa imetengwa, suala linaloonesha kwamba, siasa za Trump zimebana na kufubaza uhusiano wa nchi hiyo na waitifaki wake.
Mienendo ya Rais Donald Trump wa Marekani wakati wa mkutano wa viongozi wa G20 imekosolewa sana na wasomi, wanasiasa na vyombo vya habari. Nchi nyingi zilizoshiriki katika mkutano huo zimetoa wito wa kubadilishwa siasa za serikali ya Rais Donald Trump katika masuala mengi ikiwa ni pamoja na sera za nchi hiyo kuhusu mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Paris.