Italia yatahadharisha kuhusu kushamiri utumwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47137-italia_yatahadharisha_kuhusu_kushamiri_utumwa
Rais wa Italia ametahadharisha kuhusu kuzidi kushamiri tatizo la utumwa na magendo ya binadamu.
(last modified 2025-10-19T03:07:26+00:00 )
Jul 31, 2018 07:52 UTC
  • Italia yatahadharisha kuhusu kushamiri utumwa

Rais wa Italia ametahadharisha kuhusu kuzidi kushamiri tatizo la utumwa na magendo ya binadamu.

Rais Sergio Mattarella wa Italia alisema jana katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya Magendo ya Binadamu kuwa wahajiri wamekuwa watumwa wapya na kwamba utumwa na magendo ya binadamu ni moja ya changamoto zinazomsibu mwanadamu katika zama hizi. Rais wa Italia amesema kuwa ongezeko kubwa la idadi ya raia wanaotafuta hifadhi ni sababu ya kuibuka na kuenea kwa aina mpya ya utumwa. Amesema utumwa ni fedheha kubwa zaidi ya mwanadamu na kwamba hii leo dunia inapaswa kulaani aina zote za utumwa wa zamani na wa kisasa. 

Rais Mattarella ameongeza kuwa kila siku maelfu ya watu na familia zao huhatarisha maisha yao baharini na kwenye nchi kavu kutokana na hali ngumu ya kivita, umaskini na ukosefu wa amani, na kisha kutumbukia katika mtego wa magenge ya magendo ya binadamu sambamba na kukabiliwa na ukandamizaji na kubakwa.   

Shirika la Kazi Duniani (ILO) limeripoti kuwa karibu watu milioni 40 duniani ni wahanga wa utumwa; ambao milioni 25 kati yao wametumikishwa kwa lazima na milioni 15 wengine wameingia katika ndoa kwa kulazimishwa.