UN yaonya kuhusu kutofuatiliwa kisheria wanaojihusisha na magendo ya binadamu
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhuusiana na kutofuatiliwa kisheria watuu wanaojihusisha na biashara ya magendo ya binadamu.
Hayo yamo katika ripoti ya Umoja wa Mataifa ambayo imeonya kuhusiana na kutokuweko ufuatiliaji wa kisheria kwa watu ambao wamekuwa wakifanya magendo ya binadamu na kusisitiza kwamba, wahanga wa magendo ya binadamu wamekuwa wakikumbwa na masaibu mbalimbali kama kufanywa watumwa wa ngono na hata viungo vyao kunyofolewa na kuuzwa.
Katika hali ambayo baadhi ya watu wanaojuhusisha na biashara ya magendo ya binadamu katika nchi nyingi za Afrika na Mashariki ya Kati wametiwa mbaroni na kuhukumiwa, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Madawa ya Kulevya na Uhalifu inasisitiza kwamba, kesi za watu waliohukumiwa ni chache ukilinganisha na ukubwa wa uhalifu wenyewe.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, mwaka 2014-2017 kuliripotiwa kesi 100 za wizi wa viungo vya binadamu Mashariki ya Kati na katika eneo la kaskazini mwa Afrika. Aidha kuna ripoti za matukio kama hayo pia katika nchi za Bara Ulaya na huko Amerika ya Kati na Kusini.
Ripoti ya Ofisi ya Kupambana na Madawa ya Kulevya na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa imeeeleza kuwa, nyaraka zilizopo baada ya kufanyika uchunguzi zinaonyesha kuwa, baadhi ya wafanya magendo wamekuwa wakishirikiana na madaktari mabingwa katika upasuaji.