UN: Majiji yanatumia thuluthi mbili ya nishati yote duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56979-un_majiji_yanatumia_thuluthi_mbili_ya_nishati_yote_duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema thuluthi mbili ya nishati yote duniani inatumika katika majiji, na hivyo kuzalisha asilimia 70 ya gesi hatari ya carbon dioxide.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2019 21:47 UTC
  • UN: Majiji yanatumia thuluthi mbili ya nishati yote duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema thuluthi mbili ya nishati yote duniani inatumika katika majiji, na hivyo kuzalisha asilimia 70 ya gesi hatari ya carbon dioxide.

Antonio Guterres aliyasema hayo jana Alkhamisi, kwa mnasaba wa Siku ya Majiji Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 31 kila mwaka.

Katika ujumbe huo, Guterres amebainisha kuwa: "Zaidi ya asilimia 50 ya watu wote duniani wanaishi katika majiji na miji mikubwa na kwamba kufikia mwaka 2050, idadi hiyo itaongezeka hadi asilimia 75."

Katibu Mkuu wa UN ameeleza bayana kuwa, licha ya kuwa asilimia 80 ya mapato na uchumi wa dunia unazalishwa na majiji na miji mikubwa sawa na kuwa vitovu vya elimu, viwanda, ujasiriamali na ubunifu haswa kwa tabaka la vijana kwa upande mmoja, lakini majiji na miji hiyo imeendelea kuwa wachafuzi wakubwa wa hali ya hewa na wazalishaji wa gesi hatari kwa afya ya mwanadamu kwa upande mwingine.

Aghalabu ya viwanda duniani vinapatikana mijini

Utafiti uliotolewa mapema mwaka huu ulibainisha kuwa, uchafuzi wa hali ya hewa duniani umepelekea kuongezeka idadi ya mimba kuharibika au wanawake kujifungua kabla ya wakati.

Aidha Juni mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kuhusu ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa na taathira zake kwa viumbe kote duniani, ambapo Marekani ilitajwa kuwa ya kwanza kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda kwa kuchafua mazingira na hali ya hewa.