UN: Rasimu ya katiba mpya ya Syria kuanza kuandikwa Jumatatu
Umoja wa Mataifa umesema Kamati ya Katiba ya Syria itaanza kuandika rasimu ya katiba mpya ya nchi hiyo ya Kiarabu kesho Jumatatu.
Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres amesema anatumai kuwa, kuanza kuandaliwa rasimu ya katiba mpa ya Syria ni hatua moja mbele ya kuelekea katika mkondo wa amani ya kudumu.
Kamati hiyo ya wanachama 150 imeunda kamati ndogo ya watu 45 watakaoanza shughuli hiyo muhimu ya kutunga katibya ya Syria kesho Jumatatu.
Wajumbe15 kati yao ni wale wanaoungwa mkono na serikali ya Damascus, wengine 15 wanatoka katika makundi mengine huku 15 waliobakia wakiteuliwa kutoka katika jumuiya za kiraia.
Geir Pedersen, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria amewapongeza wawakilishi wa serikali, upinzani na mashirika ya kijamii ya Syria kwa kuketi pamoja na kufanya vikao vilivyopelekea kuzaliwa kamati hii ya katiba.
Hata hivyo mwakilishi huyo wa UN hajaainisha muda wa kufikia tamati vikao hivyo vya kuandaa rasimu ya katiba mpya ya Syria.
Jumatano iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kamati ya Katiba ya Syria ulifanyika huko Geneva Uswisi kwa kuhudhuriwa na ujumbe wa serikali, wapinzani na wawakilishi wa jumuiya za kiraia.