Vikwazo vya Marekani vimefika katika mpaka wa jinai dhidi ya binadamu
Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: "Kwa kuendeleza na kushadidisha vikwazo vyake vilivyo kinyume cha sheria, ugaidi wa kiuchumi na ugaidi wa kitiba sasa Marekani imefika katika mpaka wa jinai dhidi ya binadamu."
Majid Takht-Ravanchi, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa aliyasema hayo katika kikao cha kuchunguza "Taathira za Hatua za Upande Mmoja na za Kimabavu katika Jitihada za Kimataifa za Kukabiliana na Corona", ambacho kilifanyika Jumanne katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema: "Kupata dawa na vifaa vyote vya tiba vinavyohitajika kuzuia kuenea corona ni haki ya mataifa yote lakini hatua za upande mmoja za Marekani ni kizingiti kikubwa katika kupatikana haki hiyo."
Takht- Ravanchi ameongeza kuwa, Marekani imetoa madai yasiyo na msingi kwamba hakuna vikwazo vinavyotekelezwa katika sekta ya dawa na vifaa vya tiba. Aidha amesema vikwazo vya kimataifa vya Marekani vimezizuia nchi zingine kutumia mfumo maalumu wa kifedha na biashara ambao ulihitajika ili kupata dawa, vifaa vya tiba na bidhaa za chakula.

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuimarisha mshikamano na kwa sauti moja ilaani vikwazo vilivyo kinyume cha sheria na haramu ili janga la sasa la corona liweze kuhitimishwa kwa msingi wa thamani za kibinadamu na kimaadili.
Kikao hicho cha kuchunguza "Taathira za Hatua za Upande Mmoja na za Kimabavu katika Jitiahda za Kimataifa za Kukabiliana na Corona", kilifanyika kufuatia pendekezo la wawakilishi wa Iran, Russia, China, Venezuela, Cuba, Belaruss, Nicaragua na Zimbabwe. Mbali na mabalozi wa nchi hizo katika Umoja wa Mataifa kuhutubia, kikao hicho pia kilihutubiwa na wasomi na wanaharakati wa kimataifa.