Pelosi atetea makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, amkosoa Yair Lapid
Spika wa Kongresi ya Marekani ametetea makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya Iran na nchi za kundi la 5+1 katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa utawla haramu wa Israel mjini Washington.
Nancy Pelosi ameashiria hitilafu zilizopo baina ya Washington na Tel Aviv kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia na kukosoa jitihada kubwa zinazofanywa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya sera za Marekani katika uwanja huo na vilevile lobi za taasisi zenye mfungamano na utawala huo wa Kizayuni.
Wakati huo huo Mkuu wa Kamati ya Majeshi ya Marekani katika Kongresi ya nchi hiyo, Adam Smith ambaye pia ameshiriki katika kikao hicho, ametetea makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema yamekuwa na taathira.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa tarehe 8 Mei 2018 rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump, alichukua hatua ya upande mmoja na ya kinyume cha sheria ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuanza kutekeleza sera aliyoiita "mashinikizo ya juu kabisa" dhidi ya Iran.
Maafisa wa serikali ya sasa Marekani inayoongozwa na Joe Biden wamekiri kadhaa kuwa sera hiyo ya Trump imegonga mwamba na kudai kwamba wanataka kuirejesha Washington kwenye JCPOA; lakini hadi sasa wanakaidi kutekeleza hatua zinazohitajika ili kuweza kurejea katika makubaliano hayo.