Mgogoro wa madaraka nchini Uingereza; Boris Johnson ajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i85612-mgogoro_wa_madaraka_nchini_uingereza_boris_johnson_ajiuzulu
Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza hatimaye ametangaza rasmi kujiuzulu kwake kama kiongozi wa chama tawala cha Wahafidhina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2022 04:17 UTC
  • Mgogoro wa madaraka nchini Uingereza; Boris Johnson ajiuzulu

Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza hatimaye ametangaza rasmi kujiuzulu kwake kama kiongozi wa chama tawala cha Wahafidhina.

Chini ya miaka mitatu iliyopita, Boris Johnson aliwaongoza Wahafidhina katika ushindi mkubwa wa chama chake ambao ulikuwa haujawahi kushuhudiwa nchini tangu 1987. Pamoja na hayo, siku ya Alkhamisi Johnson alidhihiri mbele ya ofisi yake na kutangaza kujiuzulu kwake kama kiongozi wa chama tawala cha Wahafidhina na kuongeza kuwa ataendelea kuhudumu kama msimamizi wa ofisi ya waziri mkuu hadi  uchaguzi mpya utakapofanyika miezi michache ijayo.

Chama cha Wahafidhina kina wingi wa viti katika bunge, hivyo waziri mkuu mpya wa Uingereza anatarajiwa kuchaguliwa kutoka chama hicho. Kwa mujibu wa Johnson chama hicho kitafanya kikao wiki ijayo kwa ajili ya kuwasilisha mpango wa kuchaguliwa kiongozi mpya wa chama. Swali muhimu linaloulizwa ni kuwa je, licha ya ushindi mkubwa aliopata Johnson katika uchaguzi wa 2019, ni nini kimempelekea atangaze kujiuzulu na kuondoka katika ofisi yake iliyo katika jengo la 10 katika mtaa wa Downing Street?

Boris Johnson

Bila shaka "Kashfa ya Pincher"; ni moja ya sababu muhimu za kuibuka mgogoro wa madaraka wa hivi sasa nchini Uingereza. Ukweli wa mambo ni kuwa serikali ya Boris Johnson inayokabiliwa na kashfa nyingi, inapitia matatizo ya hivi sasa kutokana na tabia mbovu za Chris Pincher, naibu kiongozi wa chama cha Wahafidhina ambaye pia anasimamia utendakazi wa wabunge wa chama hicho. Pincher anashtakiwa kuwagusa kimatamanio wanaume wawili, suala ambalo limeibua tuhuma nyingi dhidi yake ambapo baadhi zinarejea nyuma miaka mingi iliyopia.

Kashafa ya kuandaliwa dhifa katika majengo ya ofisi ya Waziri Mkuu katika kilele cha kutekelezwa sheria kali za kuzuia kunea virusi vya corona, ambayo ni mashuhuri kwa jina la Partygate iliibua mawimbi makali ya ukosoaji ambapo Johnson alitakiwa ajiuzulu mara moja.

Mgogoro wa kupanda gharama ya maisha na ongezeko la kodi ni suala jingine ambalo limechangia mgogoro wa madaraka wa hivi sasa nchini Uingereza. Ughali wa maisha umeongezeka pakubwa nchini humo mwaka huu na kufikia asilimia 9.1 ambacho ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini tangu miaka 40 iliyopita. Serikali ya Johnson pia iliongeza kodi mwezi Aprili uliopita.

Keir Starmer, kiongozi wa chama cha Leba anasema: "Serikali imeamua kuongeza kodi ya mapato kwa wafanyikazi katikati ya hali mbaya zaidi ya ughali wa maisha kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa iliyopita."

Licha ya Johnson kupata uungaji mono mkubwa wa chama cha Wafidhina kwa ajili ya kufanikisha mpango wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya mashuhuri kwa jina la Brexit, lakini uungaji mkono huo haukudumu kwa muda mrefu ambapo alikabiliwa na kashfa nyingi zilizopelekea mawaziri wake mwenyewe kumkosoa vikali na hatimaye kujiuzulu serikalini.

Keir Starmer, Kiongozi wa Chama cha Leba

Pamoja na hayo mjadala uliopo hivi sasa nchini humo ni kuhusu mtu atakayechukua nafasi ya Johnson.

Waziri Mkuu mpya wa Uingereza bila shaka atachukua usukani wa nchi hiyo katika mazingira magumu ambapo serikali inakabiliwa na changamoto nyingi za ndani na nje ya nchi. Kupanda kukubwa kwa gharama ya maisha ambako kulikuwa hakujawahi kushuhudiwa tena tangu miaka 50 iliyopita, kumeiweka nchi hiyo katika hali ngumu. Pamoja na hayo lakini Uingereza inahesabiwa kuwa nchi ya pili inayotoa misaada mingi ya kijeshi kwa Ukraine, baada ya Marekani. Licha ya hayo tunapasa kusubiri na kuona ni siasa gani zitafuatwa na waziri mkuu mpya atakayechukua nafasi ya Johnson, ambaye ameitumbukiza nchi yake katika hatari kubwa ya kuweza kukabiliana moja kwa moja na Russia, jambo ambalo limeamsha hasira kubwa ya Waingereza dhidi yake.