Kukwama Ulaya na Marekani katika kinamasi huko Ukraine
Vikwazo ambavyo vililenga kumpigisha magoti Rais Vladimir Putin wa Russia na kuilazimisha nchi hiyo isitishe vita dhidi ya Ukraine vimepelekea kuongezeka bei ya nishati ya gesi kwa asilimia 700 barani Ulaya, na kuibua tetesi juu ya uwezekano wa kupanda bei ya pipa la mafuta hadi dola 380 huku masoko ya fedha nchini Marekani yakiwa yamepungua kwa asilimia 30.
Vikwazo hivyo pia vimeibua kengele ya hatari kuhusu dhoruba kubwa ya kiuchumi inayoweza kushuhudiwa barani Ulaya hivi karibuni. Ursula von der Leyen Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya akizungumza katika Bunge la Ulaya katika mji wa Strasbourg nchini Ufaransa ameashiria kengele ya hatari kuhusu uwezekano wa bara Ulaya kukumbwa na tufani ya kiuchumi iwapo Russia itasitisha kikamilifu uuzaji wa gesi yake kwa nchi za Ulaya. Bi Vo der Leyen aidha ametahadharisha kuwa Umoja wa Ulaya unahitaji mipango ya dharura ili kujiandaa iwapo Russia itasitisha kikamilifu kuziuzia nchi za Ulaya nishati ya gesi. Awali, wataalamu wa masuala ya uchumi katika Benki ya Jp Morgan ya nchini Marekani pia walitoa tathmini yao mpya na kutahadharisha kuwa kama Russia itapunguza uzalishaji wake wa mafuta ghafi kwa siku hadi mapipa milioni 5 basi bei ya mafuta kwa pipa moja huenda ikafikia dola 380 kutoka bei ya sasa ya karibu dola 110.
Masoko ya fedha nchini Marekani pia mwaka huu yameshuka kwa asilimia 30 kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta na mfumuko wa bei. Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa, bei ya umeme barani Ulaya imepanda mara nne kutokana na kupanda kwa bei ya nishati ya gesi huku gazeti la Bloomberg pia likiripoti kuwa, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, bara Ulaya hivi sasa linakabiliwa na kupanda kwa bei ya gesi kwa karibu asilimia 700 kulinganisha na mwaka uliopita.
Moja ya sababu kuu zilizoibua hali ya sasa ya nishati duniani ni vita vya Ukraine; ambapo Russia ikiwa moja ya nchi wazalishaji wakuu wa nishati duniani imekumbwa na vikwazo vya Magharibi kwa kuanzisha vita dhidi ya nchi hiyo. Marekani na Ulaya tokea Februari 24 mwaka huu sambamba na kuanza mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukarine zimewawekea vikwazo viongozi wa Russia, taasisi na makampuni kadhaa ya nchi hiyo; na hivyo kuifanya Russia kuwa nchi iliyokumbwa na vikwazo vingi duniani katika kipindi cha wiki kadhaa tu. Aidha lengo la vikwazo hivyo vya nchi za Magharibi dhidi ya Moscow pia ilikuwa wazi kikamilifu tangu awali yaani kutoa pigo kwa Vladimir Putin na kuizuia nchi hiyo kuendelea na vita huko Ukraine. Hata hivyo licha ya vikwazo vyote hivyo tajwa imeelezwa kuwa, vita vingali vinaendelea huko UKraine na Russia pia hivi karibuni imetangaza kuudhibiti kikamilifu mkoa wa Luhansk unaopatikana mashariki mwa Ukraine.
Wakati huo huo vikwazo katika sekta kama ya nishati hata vimeishia kwa maslahi ya Russia sambamba na nchi hiyo kudhibiti aghalabu ya maeneo ya kimkakati huko kusini na mashariki mwa Ukraine. Wakala wa Kimataifa wa Nishati umetangaza kuwa, uzalishaji wa mafuta ghafi wa Russia mwezi mei mwaka huu uliongezeka kwa karibu mapipa milioni 10 na 550,000 kwa siku. Hii ina maana kwamba, Russia imepata ongezeko la asilimia 11 la mapato yake kutokana na uuzaji wa mafuta mwezi Mei mwaka huu ikilinganishwa na mwanzoni mwa mwaka uliopita na kufikia karibu dola bilioni 20.
Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya hivi karibuni amekiri kuhusu hali mbaya ya kiuchumi na kupanda kwa bei ya nishati barani Ulaya na kudai kuwa "mgogoro wa nishati ambao unahisika katika nchi za Ulaya ni gharama ambayo inapaswa kulipwa na umoja huo ili kulinda demokrasia na kuhitimishwa satwa ya Russia kwa maamuzi ya kisiasa ya Brussels."
"Dmitry Medvedev Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia Jumatano iliyopita aliitaja mitazamo na fikra za nchi za Magharibi za kutaka kuiadhibu Russia kuwa ni za kipumbavu na zisizo na maana na akahoji, ni nani anapiga kelele kwamba Russia ni lazima ifikishwe mbele ya vyombo vya sheria na kuhukumiwa? Ni yule ambaye anaua watu bila hatia bila ya kuhukumiwa huku akiendelea kutenda jinai za kivita, ni wale ambao hata hivyo hawana ukosoaji wowote wa kweli katika miundo ya kimataifa wanaoifadhili kifedha."
Medvedev ameeleza hayo akiashiria utafiti uliofanywa na Taasisi ya Global Research ambapo kwa mujibu wa utafiti huo, tokea kumalizika Vita vya Pili vya Dunia hadi sasa Marekani imeua zaidi ya watu milioni 20 katika nchi 37 duniani. Huenda dunia hivi sasa isingekuwa katika hali ya mizozo na machafuko iwapo taasisi za kimataifa zisingezembea kuchukua hatua mkabala wa jinai ambazo zilitekelezwa na Marekani na waitifaki wake huko Vietnam, Iraq, Afghanistan, Syria na maeneo mengine duniani.