Mauaji ya Srebrenica ni aibu kwa madola ya Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i85784-mauaji_ya_srebrenica_ni_aibu_kwa_madola_ya_magharibi
Katika maadhimisho ya miaka 27 ya mauaji ya halaiki ya Srebrenica, makumi ya maelfu ya watu walitembea kilomita mia moja hadi Srebrenica kuwakumbuka wahasiriwa wa moja ya mauaji makubwa zaidi ya kimbari barani Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 13, 2022 02:14 UTC
  • Mauaji ya Srebrenica ni aibu kwa madola ya Magharibi

Katika maadhimisho ya miaka 27 ya mauaji ya halaiki ya Srebrenica, makumi ya maelfu ya watu walitembea kilomita mia moja hadi Srebrenica kuwakumbuka wahasiriwa wa moja ya mauaji makubwa zaidi ya kimbari barani Ulaya.

Wakati wa hafla hiyo, mabaki yaliyotambuliwa upya ya waathirika 50 wa maafa ya Srebrenica walizikwa pamoja na wengine 6,671 kwenye Makaburi ya Kumbukumbu ya Srebrenica.

Taasisi za kimataifa zilitangaza mauaji hayo ya kikatili kuwa mauaji makubwa zaidi ya kimbari katika historia ya Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia, lakini nukta inayoumiza zaidi ya mauaji hayo ya kinyama ni shambulio na mauaji ya wanaume na wanawake ambao walikuwa wamekimbilia katika mji wa Srebrenica chini ya ulinzi wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa.

Saeeda Bagherifard, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Kitamaduni ya Wanawake ya Iran ameshiriki katika ufunguzi wa maonyesho yaliyofanyika Tehran ya picha yaliyopewa anwani ya "Mawe Meupe, Mioyo Isiyotulia" kwa mnasaba wa mwaka wa 27 wa maafa ya Mauaji ya Kimbari ya Waislamu wa Srebrenica na kusema: Licha ya kuwepo madai yote ya Wamagharibi ya kutetea haki za kibinadamu, katika hatua ya kusikitisha, Vikosi vya Umoja wa Mataifa viliwaacha mikononi mwa maadui wanaume, wanawake na watoto waliopokonywa silaha. Unyama huo uliotokea katika zama hizi, ambapo mashirika ya haki za binadamu duniani yanajaribu kuuficha na kuusahau.

Julai 11, 1995 ni siku ya aibu na majuto kwa serikali za Ulaya zinazodai kutetea ubinadamu. Siku hii, msiba mkubwa wa kibinadamu ulitokea katikati ya Ulaya na serikali za Ulaya zilikuwa zikiutazama tu. Serikali za Ulaya zimekuwa zikijitahidi kadiri zinavyoweza kuficha na kupuuza janga hili la kibinadamu. Waserbia wabaguzi wa Bosnia walifanya uhalifu na mauaji makubwa ya kimbari ya Waislamu wa Bosnia kati ya 1992 na 1995 na kuua makumi ya maelfu ya Waislamu Wabosnia wakiwemo wanawake, watoto, wanaume na vijana. Srebrenica ni kilele cha uhalifu wa Waserbia wahalifu chini ya uongozi wa watenda jinai Radovan Karadzic na Ratko Mladic na kwa msaada wa dikteta wa Yugoslavia Slobodan Milosevic na kwa uungwaji mkono wa Ufaransa na Uingereza.

Ratko Mladic mmoja wa watenda jinai wakuu katika mauaji ya Srebrenica

Katika miezi ya mwisho ya mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Bosnia na katika mwaka wa tatu wa mauaji hayo ya kimbari, Umoja wa Mataifa ulitangaza miji mitatu ya Bosnia na Herzegovina kuwa maeneo salama ili kuwaweka raia Waislamu ili wasishambuliwe na wahalifu makatili. Moja ya miji hiyo ulikuwa mji wa Srebrenica. Walinda amani 400 wa Umoja wa Mataifa wa Uholanzi walikuwa wakiulinda mji huo. Maelfu ya Wabosnia waliokimbia makazi yao walifika Srebrenica kwa dhana kuwa mji huo ulikuwa salama kwao. Lakini Ratko Mladic, mmoja wa viongozi wa uhalifu wa Waserbia wa Bosnia, aliizingira Srebrenica akiwa na wanajeshi 2,000, bila kujali sheria za kimataifa. Mladic alichukua hatua hiyo wakati walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa Uholanzi walikuwa na fursa ya kutosha kuripoti kwa serikali zao na maafisa wa Umoja wa Mataifa na kuomba msaada wa dharura.

Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi Kajsa Ollongren amewaomba msamaha Waislamu wa Bosnia na ameshiriki  katika ibada ya kumbukumbu ya 27 ya waathirika wa mauaji ya kimbari ya Srebrenica. Hata hivyo, maneno aliyotumia waziri huyo wa Uholanzi kuomba radhi yanaonyesha kwamba lengo lake lilikuwa tu  kusafisha jina la  walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa Uholanzi kuliko kuomba msamaha. Alidai kwamba wanajeshi wa Uholanzi walifanya kila wawezalo kutimiza malengo yao ya kuwatetea watu wasio na hatia wa Srebrenica. Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi alisema kwamba maumivu ya mauaji hayo hayatafutika kamwe na kuongeza kuwa ni Waserbia wa Bosnia ndio walihusika na maafa hayo na kwamba wengi wao walihukumiwa katika mahakama za kimataifa.

Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi Kajsa Ollongren katika kumbukizi ya  maafa ya Srebrenica

Hata hivyo  maneno ya walionusurika katika maafa ya Srebrenica na matokeo ya uchunguzi wa kamati za kutafuta ukweli zilizoundwa baada ya maafa ya Srebrenica yanaonyesha kuwa madai ya Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi hayana ukweli wowote.