UN yaitaka Marekani izipe fidia familia za wahanga wa utumwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i87666-un_yaitaka_marekani_izipe_fidia_familia_za_wahanga_wa_utumwa
Umoja wa Mataifa umetoa mwito kwa Marekani kuanza mchakato wa kutoa fidia kwa vizazi vya wahanga wa utumwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2022 03:01 UTC
  • UN yaitaka Marekani izipe fidia familia za wahanga wa utumwa

Umoja wa Mataifa umetoa mwito kwa Marekani kuanza mchakato wa kutoa fidia kwa vizazi vya wahanga wa utumwa.

Kamati ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi ya Umoja wa Mataifa imesema hayo na kuongeza kuwa, athari za ukoloni na utumwa zinaendelea kuchochea ubaguzi wa rangi nchini Marekani, jambo ambalo linafanya haki za binadamu na za msingi za watu na jamii za nchi hiyo zikanyagwe.

Ripoti ya kamati hiyo ya UN imeitaka Kongresi ya Marekani ipasishe muswada wa mwakilishi wa Texas kwa tiketi ya Democrat, Sheila Jackson Lee, unaotaka kuundwa kamati ya kufuatilia masuala ya kulipwa fidia wahanga wa utumwa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamepongeza mwito huo wa Kamati ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi ya Umoja wa Mataifa wa kuitaka Washington kuwapa fidia jamaa za wahanga wa utumwa nchini Marekani.

Watumwa wa enzi wanavyotumikishwa katika nchi za Magharibi

Kamati ya Kupambana na Ubaguzi wa Rangi ya UN imeongeza kuwa, uhalifu wa kutumia silaha moto unawaathiri zaidi watu wa jamii za waliowachache Marekani, hususan wenye asili ya Afrika, ikiwa ni sehemu ya athari za utumwa na ukoloni.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, watu zaidi ya milioni 40 kote duniani ni wahanga wa utumwa mamboleo, huku wanawake na wasichana miongoni mwao wakitumika kama watumwa wa ngono.