ILO yatoa indhari: Fursa za ajira duniani zinazidi kupungua
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani, ILO limetoa ripoti yake inayotahadharisha kuwa ukosefu wa ajira na ukosefu wa usawa vyote vitaendelea kuongezeka duniani kutokana na majanga lukuki yanayoingiliana ya kiuchumi na kisiasa na hivyo kutishia kukwamuka kwa soko la ajira ulimwenguni.
Ripoti hiyo iliyotolewa jana mjini Geneva, Uswisi inaonesha kuwa mwelekeo wa soko la ajira duniani umekuwa mbaya zaidi katika miezi ya karibuni na mwelekeo wa nafasi za ajira utapungua sambamba na kiwango cha ukuaji wa ajira duniani kwenye robo ya mwisho ya mwaka huu wa 2022 iliyoanza mwezi uliomalizika wa Oktoba.
Ripoti hiyo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani iliyotolewa kwa anuani “Ufuatiliaji wa Sekta ya Ajira Duniani”, inasema vita vya Ukraine pamoja na ongezeko la mfumuko wa bei vinasababisha kuporomoka kwa viwango halisia vya ujira kwenye nchi nyingi duniani, na hii inaambatana na kuporomoka kwa ujira kwa kiasi kikubwa wakati wa janga la COVID-19 ambalo limeathiri zaidi makundi ya kipato cha chini.
Ukosefu wa ajira unadhihirika zaidi madhara yake kwenye ongezeko la bei za vyakula na nishati, huku uchumi ukidorora na fursa za maboresho ya kisera zikipungua.
Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert Houngbo amesema majawabu ya kutatua hali ya sasa ya ajira na kuepusha hali kuwa mbaya zaidi yanahitaji sera za kina na zinazoingiliana na ambazo pia zina mizania kitaifa na kimataifa.
Houngbo amesema “tunahitaji utekelezaji wa sera nyingi na pana ikiwemo sera za kuingilia kati kupunguza bei za vyakula, kugawana vyema mapato ambayo hayakutarajiwa, kuimarisha hifadhi ya jamii na sera mahsusi za kulenga watu walio hatarini zaidi…/