Kuendelea kunyongeshwa Waislamu wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i92002-kuendelea_kunyongeshwa_waislamu_wa_rohingya
Jeshi la Majini la Sri Lanka limetangaza kuwa, limeokoa Waislamu 104 wa jamii ya Rohingya katika fukwe za kaskazini mwa Bahari ya Hindi wakati walipokuwa wanakimbia mateso nchini kwao Myanmar.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Dec 22, 2022 23:14 UTC
  • Kuendelea kunyongeshwa Waislamu wa Rohingya

Jeshi la Majini la Sri Lanka limetangaza kuwa, limeokoa Waislamu 104 wa jamii ya Rohingya katika fukwe za kaskazini mwa Bahari ya Hindi wakati walipokuwa wanakimbia mateso nchini kwao Myanmar.

Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa Waislamu wa jamii ya Rohingya wanateseka kutokana na ukatili mkubwa wanaofayiwa nchini kwao Myanmar. Waislamu hao wamelazimika kuwa wakimbizi katika nchi na maeneo tofauti hasa Bangladesh. Wanapitia mazingira magumu sana njiani na kwenye maeneo wanakokimbilia. Wanalazimika kukimbia nchini kwao Mynamar wakiwa wameacha kila kitu isipokuwa nguo zao za mwilini na wanaishi kwenye mazingira duni yenye huduma za chini kabisa za chakula, malazi na matibabu. Zaidi ya hayo serikali ya Bangladesh imetangaza kuwa, itawapeleka baadhi ya wakimbizi wa Rohingya katika kisiwa cha mbali kisicho na suhula zozote, suala ambalo limezidi kuwatia unyonge Waislamu hao. Sababu yake ni kuwa, kisiwa hicho cha mbali sana, ni sehemu ya kutupwa watu na si sehemu ya kuishi wanadamu wa kawaida. Hakuna njia na namna yoyote ya kuweza kutoka kwenye kisiwa hicho. Ni kwa sababu hiyo ndio maana taasisi mbalimbali za kimataifa za kijamii zimetoa onyo kali kwa serikali ya Bangladesh, isichukue hatua kama hiyo. Lakini Bangladesh nayo ni nchi maskini yenye matatizo chungu nzima ya kijamii, kiusalama na kiuchumi ambayo hivi sasa yameongezeka kwa kuvamiwa na wimbi kubwa la wakimbizi hao yaani Waislamu wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar. Serikali ya Bangladesh inaitaka jamii ya kimataifa iisaidie kuwatunza wakimbizi hao, lakini haipewi msaada wa kutosha.

UN: Waislamu wa Rohingya ndiyo jamii ya wachache inayodhulumiwa zaidi duniani

 

Roui Sefat, ni mtaalamu wa masuala ya kimataifa ambaye anasema: Zaidi ya Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya wanaishi kama wakimbizi katika mji wa Cox’s Bazar wa kusini mashariki mwa Bangladesh. Wakimbizi hao hawana shuhula zozote za kuendeshea maisha. Wanalazimika kuishi katika mazingira hayo magumu baada ya kulazimishwa kukimbia makazi yao nchini Myanmar na kupoteza kila walichokuwa wanamiliki. Hakuna matumaini yoyote ya kuboreka hali ya wakimbizi hao. Kushindwa serikali ya Bangladesh kuwasaidia wakimbizi hao na kutoweza kuboresha hali yao ya maisha, kunazidi kuwatia unyonge Waislamu hao wa jamii ya Rohingya.

Kabla ya hapo serikali ya Bangladesh ilikuwa imefikia makubaliano na serikali ya Myanmar ya kuhakikisha wakimbizi hao wanarejea katika maeneo yao kwenye mkoa wa Rakhine baada ya hali kutulia na mambo kuwekwa sawa. Lakini serikali ya Myanmar si tu imepuuza makubaliano hayo bali pia inazidi kuwashinikiza Waislamu hao wanaodhulumiwa kila upande na kuwalazimisha kukimbia makazi yao wakiwa hohe hahe. Umoja wa Mataifa umesema kuwa, Waislamu wa Rohingya ndiyo jamii ya wachache inayodhulumiwa zaidi duniani hivi sasa. Lakini serikali ya Myanmar haioneshi kuguswa na mateso wanayopata Waislamu hao na ndio kwanza inazidisha mashinikizo dhidi yao.

Kambi ya wakimbizi ya Cox’s Bazar kusini mashariki mwa Bangladesh

 

Dk Iqbal, mtaalamu mwingine wa masuala ya kimataifa anasema: Waislamu wa Rohingya ambao hivi sasa wametelekezwa na wanateseka kwa matatizo chungu nzima ya kiafya, kimatibabu, lishe duni n.k, wanaishi kama wafungwa kwenye kambi za wakimbizi. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, lazima watatafuta maisha bora kwenye nchi jirani lakini suala hilo nalo linatishia usalama wao na hatari ya kutumbukia kwenye makucha ya magenge ya magendo ya binadamu.

Alaakullihaal, Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaendelea kudhulumiwa na kunyongeshwa licha ya taasisi za kimataifa za nchi za Magharibi kujigamba kuwa zinapigania maslahi yao. Hakuna hatua zozote za maana zilizochukuliwa hadi sasa za kuboresha hali yao duni mno katika kambi za wakimbizi. Dharau hiyo ya jamii ya kimataifa imezidi kuwapandisha kiburi viongozi wa Myanmar na kuwapa uthubutu wa kuzidisha mashinikizo yao tena kijeuri dhidi ya Waislamu wa Rohingya na bila ya kujali chochote. Ni kimya hicho cha jamii ya kimataifa ndicho kilichopelekea dunia kushuhudia mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Myanmar. Cha kusikitisha zaidi ni kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC nayo licha ya kwamba ndiyo taasisi kubwa zaidi ya kimataifa baada ya Umoja wa Mataifa, imeshindwa kulishughulikia ipasavyo suala la Waislamu hao wa jamii ya Rohingya. 

Mwanamke wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya na mwanawe mchanga, wametelekezwa, hawajui cha kufanya