Apr 02, 2023 02:29 UTC
  • Ughali wa maisha Uingereza: Wafanyakazi wa usalama wa Heathrow wagoma

Wafanyikazi wa usalama wa Uwanja wa Ndege wa Heathrow mjini London nchini Uingereza wameanzisha mgomo wa siku 10, wakiungana na wafanyakazi wengine wa serikali na wafanyikazi wa sekta kadhaa nchini humo ambao wamegoma wakitaka nyongeza kubwa ya mishahara kutokana na mfumuko wa bei unaozidi kuongezeka.

Takriban maafisa usalama 1,400 wanashiriki katika mgomo huo ulioanza Ijumaa, baada ya mazungumzo ya dakika za mwisho na maafisa wa serikali kuhusu nyongeza ya mishahara kushindwa.

Mgomo huo unahusisha wafanyakazi wa Terminal Five ya uwanja huo wa ndege, ambao unatumiwa na Shirika la Ndege la British Airways pekee. Aidha maafisa wanaohusika na kukagua mizigo iliyoingizwa kwenye uwanja huo pia wamegoma.

Mgomo huo umesababisha shirika la ndege la British Airways kufuta takriban asilimia 5 ya safari zake za ndege katika kipindi cha Pasaka, na safari 70 za ndege siku ya Ijumaa huku uwanja wa ndege ukionya kuwa baadhi ya abiria huenda wakakabiliwa na ucheleweshaji wakati wa ukaguzi wa usalama katika siku za mgomo.

Uwanja huo wa ndege umelazimika kupeleka wafanyikazi 1,000 wa ziada kufidia mgomo huo na kusaidia abiria siku ya Ijumaa.

Bango katika mgomo wa wauguzi Uingereza

Sekta ya usafiri wa anga nchini Uingereza iko chini ya shinikizo huku erikali ikifanya jitihada za kuepusha kurudiwa kwa foleni za Pasaka za mwaka jana ambazo zilisababishwa kwa kiasi kikubwa na uhaba wa wafanyikazi.

Sekta nyingi nchini Uingereza sasa zinasumbuliwa na migomo ya mamia ya maelfu ya wafanyakazi ambao wanataka mishahara bora huku bei za bidhaa na bili za nishati zikipanda.

Uwanja wa ndege wa Heathrow unadai kwamba ulikuwa umetoa nyongeza ya asilimia 10 ya mishahara kwa wafanyakazi kuanzia Januari. Hata hivyo, ofa hiyo ilikataliwa na wafanyikazi kwani ongezeko hilo halikuweza kuendana na mfumuko wa bei unaoshadidi kote Uingereza.

Mgomo wa vikosi vya usalama vya Heathrow unakuja baada ya migomo ya nchi nzima katika ‘siku ya bajeti’, wakati wafanyakazi wapatao nusu milioni wa Uingereza walipogoma huku vyama vya wafanyakazi vikiandaa matembezi makubwa kupinga bajeti ya mwaka ya Waziri wa Fedha, Jeremy Hunt.

Kama ilivyotazamiwa hapo awali, Rishi Sunak, Waziri Mkuu wa Uingereza amekumbana na changamoto nyingi za ndani na kutoka nje baada ya kuingia madarakani; kubwa kuliko zote ikiwa ni jitihada anazopasa kufanya ili kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi unaoitesa nchi hiyo pamoja na mfumuko mkubwa wa bei ambao umepindukia asilimia 10 na kupelekea kuongezeka gharama za maisha hususan katika uga wa nishati.

Tags