Ombi la Ujerumani kwa Uchina kuhusu vita vya Ukraine
Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz, ameiomba China kutumia ushawishi wake kwa Russia kusaidia jitihada za kukomesha vita nchini Ukraine.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa China, Li Qiang, Scholz amesema: "Kwa mara nyingine tena nimeiomba serikali ya China kutumia ushawishi wake kwa Russia kuhusiana na vita vya Ukraine. China ina jukumu maalumu sana kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hii ni pamoja na kwamba China ilitangaza hapo awali kuwa iko tayari kusaidia juhudi za kumaliza mgogoro wa Ukraine kwa kuwasilisha mpango wa amani wenye vifungu 12, lakini nchi za Magharibi hasa Marekani ndizo zinazoendelea kupiga ngoma ya vita huko Ukraine kwa kukataa mpango wa amani wa China.
Ombi hili la Kansela wa Ujerumani kwa China kusaidia kutatua mzozo wa Ukraine linaonyesha kuwa, Umoja wa Ulaya, haswa nchi muhimu za bara hilo, zinasumbuliwa na matatizo makubwa katika kuendeleza vita nchini Ukraine na zina wasiwasi kwamba upinzani dhidi ya vita hivyo katika nchi za Ulaya unaongezeka zaidi na unaweza kuwa na athari mbaya sana kwa shughuli za vyama tawala, ikiwa ni pamoja na huko Ujerumani. Abolfazl Zohrevand, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema: "Nchi za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ujerumani, hazikufikiria kuwa mzozo wa Ukraine ungeendelea kwa muda mrefu. Zilidhani kwamba himaya na misaada ya pande zote ya nch hizo kwa Ukraine, ingeilazimisha Russia kusalimu amri, lakini gharama kubwa za vita vya Ukraine kwa nchi za Ulaya zimezilazimisha kuipigia magoti China ili itumie ushawishi wake kwa Russia na kuuokoa Umoja wa Ulaya kutoka kwenye kinamasi cha vita vya Ukraine."
Ukweli ni kwamba nchi za Magharibi haziko tayari kutumia nafasi ya China kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Ukraine, kwa sababu zinaona kuwa suala hilo litaimarisha hadhi na nafasi ya China kimataifa. Hata Umoja wa Ulaya, hasa Ujerumani, unahisi kwamba umetumbukia katika mtego wa Marekani katika mgogoro wa Ukraine. Kwa msingi huo, unajaribu kutumia njia zote zinazowezekana, hata kwa kumpigia magoti mpinzani wake mwenye nguvu wa Mashariki, kwa ajili ya kujinasua kwenye mtego huo. Hamu iliyoonyeshwa hivi majuzi ya Russia ya kufanya mazungumzo kuhusu mgogoro wa Ukraine imezifanya nchi za Ulaya zitambue kwamba, Marekani ndiyo inayochochea kuni katika moto wa vita vya Ukraine kwa kusisitiza sera zake za kujitanua na za kibeberu.
Xi Feng Li, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: "China inafuatilia kwa dhati sera ya kurejesha amani katika kanda hiyo na hadi sasa imewasilisha mpango wake wenye vipengele 12 kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Ukraine. Hata hivyo, kutokana na uchanganuzi usio sahihi, nchi za Magharibi zimeituhusu China kuwa inaiunga mkono Russia na kupuuza mpango wake wa amani. Pamoja na hayo, kadiri muda unavyosonga mbele, nchi hizi za Magharibi zimezoonyesha kwamba haziwezi kuendeleza mgogoro wa Ukraine."
Kwa vyovyote vile, Kansela wa Ujerumani ameiomba China kutumia ushawishi wake kwa ajili ya kutatua mzozo wa Ukraine, ilhali hapo awali alidai, wakati wa mazoezi ya kijeshi ya NATO, kwamba wanachama wa shirika hilo wamejipanga kikamilifu kukabiliana na tishio lolote kutoka Russia.
Alaa kulli hal, kwa kutilia maanani nafasi na mchango muhimu wa China kimataifa, na athari haribifu za kiuchumi na kifedha za vita vya Ukraine hasa kwa nchi za Ulaya, nchi kama Ujerumani imeelewa ukweli kwamba sambamba na kuthibitisha nafasi ya China, inapaswa kuiomba ifanye juhudi za kutatua mgogoro wa Ukraine ili zisizame na kutumbukia zaidi kwenye kinamasi cha vita vya Ukraine.