Nchi za Ulaya zabadili mtazamo kuhusu kundi la kigaidi la Munafikina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i99132-nchi_za_ulaya_zabadili_mtazamo_kuhusu_kundi_la_kigaidi_la_munafikina
Nchi za Ulaya ambazo zimekuwa mwenyeji wa makundi ya kigaidi na ya uasi dhidi ya Iran tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hivi karibuni zimechukua hatua zinazoashiria kuwepo mabadiliko katika mtazamo wao kuhusu makundi hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2023 23:00 UTC
  • Nchi za Ulaya zabadili mtazamo kuhusu kundi la kigaidi la Munafikina

Nchi za Ulaya ambazo zimekuwa mwenyeji wa makundi ya kigaidi na ya uasi dhidi ya Iran tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hivi karibuni zimechukua hatua zinazoashiria kuwepo mabadiliko katika mtazamo wao kuhusu makundi hayo.

Licha ya miaka mingi ya uungaji mkono wa wazi na wa siri wa nchi za Magharibi, hasa za Ulaya, kwa kundi la kigaidi la Munafika ambapo zimewapa makazi wanachama wa kundi hilo nchini Albania, sasa inaonekana ni kana kuwa nchi hizo zina mtazamo tofauti kuhusu kundi hilo.

Kuhusiana na hilo, Jumanne asubuhi, polisi wa Albania walishambulia makao makuu ya kundi la kigaidi la Munafikina katika mji wa pwani wa Durres, unaojulikana kama makao makuu ya Ashraf 3, na kuwatia mbaroni magaidi zaidi ya 70 ambapo gaidi mmoja aliuawa kwa kuwashambulia polisi. Mkuu wa polisi wa Albania alisema maafisa 15 wa polisi walijeruhiwa katika mapigano na wanachama wa Munafikina.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Albania pia ilitangaza kupitia taarifa kuwa operesheni hiyo ilifanyika kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia hukumu ya Mahakama ya Juu dhidi ya ugaidi. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na kundi hilo la magaidi mwaka 2014, wanachama wake wametambulika kuwa wakimbizi nchini humo kutokana na sababu za kibinadamu tu. Taarifa hiyo inaendelea kusema kuwa wanachama wa kundi hilo wamekiuka makubaliano yaliyofikiwa kwa kufanya shughuli za kigaidi na mambo mengine yanayovunja sheria mitandaoni. Baadhi ya vifaa vya kielektroniki visivyo vya kawaida zikiwemo ndege kadhaa zisizo na rubani, vilikamatwa na polisi. Katika ukaguzi huo vikosi vya usalama vilikabiliwa na upinzani na mashambulizi kutoka kwa baadhi ya wanachama wa wa Munafikina. Kufuatia shambulio dhidi ya kambi ya kundi hilo huko katika mji wa Durres, maafisa wa Albania sasa wanawafuatilia kisheria wanachama sita wa kundi hilo. Beldar Cuci, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Albania, amesema, tabia ya wanachama wa Munafikina ni ya kusikitisha na dharau kwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya nchi hiyo na kundi hilo.

Polisi wa Albania wakivamia kambi ya Munafikina

Wanachama wa Munafikina walikaribishwa nchini Albania kwa ushirikiano wa Marekani na wanachama wengine wa shirika la kijeshi la NATO baada ya kufukuzwa kutoka Iraq. Safari ya John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Marekani huko Albania mnamo Februari 14, 2014 ilifanikisha makubaliano ya siri ya kuhamishwa hadi wanachama 3,000 wa kundi hilo kwenda kuishi mjini Tirana. Mchakato wa kuhamishwa wanachama wa Munafikina kwenda Albania ulipata kasi aada ya hapo na kufikia mwishoni mwa wa Desemba 2017, kulingana na takwimu zisizo rasmi, karibu wanachama 3250 wa kundi hilo la kigaidi walikuwa tayari wameingia nchini humo. Viongozi wa Munafikina hawajioni kuwa wakimbizi katika ardhi ya Albania, bali wageni wa Marekani, na hivyo wanawahadaa wanachama wao kwamba wao ni wageni wa Pentagon na kulitumia suala hilo kama alama ya mafanikio makubwa kwao.

Ingawa wanachama wa Munafikina wanachukuliwa kuwa wageni kwa sababu za kibinadamu kulingana na madai ya serikali ya Albania, lakini walikuwa wamegeuza makao makuu ya Ashraf 3 huko Durres kuwa kituo cha kutekelezea shughuli za uhalifu wa kimtandao na shughuli nyingine za kigaidi. Kundi hilo la wanafiki limefanya vitendo vingi vya kijasusi na hujuma dhidi ya watu wa Iran kupitia mashirika yao huko Albania. Wakati huo huo, uwepo mkubwa wa kundi hilo la wanafiki nchini Albania kwa hakika unaisababishia nchi hiyo hatari kubwa ya kiusalama. Inaonekana kwamba serikali ya Albania imefikia uamuzi kwamba uwepo wa kundi hilo kaika ardhi yake si tu ni hatari kwa maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo, bali unaweza kuhatarisha pia usalama wa eneo zima. Moja ya matokeo hasi ya uwepo wa kundi hilo la wanafiki nchini Albania ni kudhoofishwa usalama wa taifa na utawala wa sheria nchini. Hatari nyingine ya kuwakaribisha wanafiki katika ardhi ya Albania ni kujumuika na kushirikiana kwao na makundi mengine ya kigaidi, kimafia, kitakfiri na kiwahabi.

Bila shaka, mabadiliko ya mbinu na siasa mpya za nchi za Ulaya dhidi ya kundi la Munafikina haziishii nchini Albania pekee, bali inaonekana kwamba Ufaransa, ambayo imekuwa msaidizi na kimbilio kuu la muda mrefu la magaidi hao, nayo imeanza kutekeleza mbinu mpya katika uwanja huo. Kuhusiana na hilo, mkusanyiko wa kila mwaka wa kundi la Munafikina nchini Ufaransa umepigwa marufuku na tayari viongozi wanaoandaa mkusanyiko hao kila mwaka walikwishaandikiwa barua kuhusiana na marufuku hiyo. Kila mwaka, tarehe 20 Juni sambamba na siku ya kuanza shughuli zake za kigaidi, kundi hilo la Munafikina limekuwa likifanya mikusanyiko yake nchini humo, lakini mwaka huu, mkutano uliokuwa ufanyike huko katika mji wa Villepinte umefutiliwa mbali kwa amri ya serikali. Polisi wa Ufaransa wamesema mkutano huo umefutiliwa mbali kutokana na matatizo ya kiusalama na kuvurugwa utulivu wa umma. Marufuku ya mkusanyiko huo wa kila mwaka, imetekelezwa kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Mmoja wa viongozi wa Munafikina akiwa na viongozi wa Magharibi ambao wana chuki kubwa dhidi ya Uislamu

Shirika la habari la Reuters limesema marufuku hiyo imetekelezwa sanjari na juhudi za nchi za Magharibi za kupunguza mvutano na serikali ya Iran na kuwa imetangazwa ikiwa zimepita wiki chache tu baada ya nchi za Ulaya na Iran kubadilishana wafungwa na pia wiki mbili baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kufanya mazungumzo ya simu ya dakika 90 na Rais Ebrahim Raisi wa Iran. Katika mazungumzo hayo, Raisi alizungumzia upotoshaji unaofanywa na baadhi ya serikali za Ulaya kuhusu taifa la Iran, na kusema ni matokeo ya serikali hizo kunaswa katika mtego wa taarifa za uwongo za makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga na yenye chuki dhidi ya mfumo wa Kiislamu. Alisisitiza juu ya udharura wa kuepuka kuingiliwa masuala ya ndani ya Iran na kuheshimiwa msingi wa mataifa kujitawala.