John Kerry na kukanusha ukweli usiopingika
-
John Kerry
John Kerry, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani katika utawala wa Barack Obama na ambaye ni mwakilishi maalumu wa Washington katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, amezungumzia kile amekitaja kuwa uvamizi wa kijeshi wa Russia huko Ukraine katika mahojiano na televisheni ya Ufaransa.
Alipoambiwa na mwandishi wa habari wa Ufaransa kuwa kile kilichofanyika huko Iraq pia ulikuwa uvamizi wa kijeshi, aliruka na kusema: "Hapana, haukuwa uvamizi wa kijeshi kwa sababu hakuna mashtaka ya moja kwa moja yaliyoelekezwa dhidi ya rais wa wakati huo wa Marekani George Bush." Akijibu swali la mwandishi wa kanali ya LCI kuhusu iwapo vita vya Iraq vilikuwa jinai ya kivita, John Kerry amedai, "Hutuwezi kusema ilikuwa jinai, bila shaka kulikuwa na makosa yaliyofanyika katika vita hivyo na mimi nilizungumza na kuyalalamikia.”
Kulingana na uchunguzi wa maoni uliofanywa, uvamizi wa Bush na Blair na kukaliwa kwa mabavu Iraq kulisababisha vifo vya zaidi ya raia milioni moja wa nchi hiyo ya Kiarabu. Vikosi vya Marekani vilifanya jinai kubwa za kivita, ikiwa ni pamoja na kuteswa askari waliotekwa. Katika jela ya kuogofya ya Abu Ghraib karibu na mji mkuu, Baghdad, maafisa wa Marekani walitesa na kuwadhalilisha wafungwa wa Iraq kinyume na Mkataba wa Geneva. Uvamizi huo ulikabiliwa na mapambano ya Wairaki, lakini mbinu za kukabiliana na uasi za Marekani zikiwemo za kuvamia na kuwatesa wakazi wa vijijini zilisababisha mauaji ya raia wengi wasio na silaha.
Ulimwengu ulipinga vita hivyo vya Bush na Blair lakini kwa masikitiko makubwa haukufanya lolote kukabiliana navyo. Hakuna serikali yoyote iliyoziwekea vikwazo serikali za Marekani na Uingereza. Makama ya Kimataifa ya Jinai ICC haikutoa waranti wowote wa kukamatwa viongozi hao wa Marekani na Ungereza kutokana na jinai za kutisha zilizotekelezwa dhidi ya watu wa Iraq wasio na hatia.
Lakini hivi sasa nchi za Magharibi zimechukua msimamo tofauti kuhusu vita vya Ukraine, ambao ni mfano mwingine wa wazi wa siasa za ubaguzi na undumakuwili unaofanywa na nchi hizo kuhusu masuala ya kimataifa, undakuwili ambao umedhihirika wazi zaidi katika matamshi ya karibuni ya John Kerry.
Uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Marekani na Uingereza dhidi ya Iraq ni uvamizi uliofanyika nje ya sheria za kimataifa na idadi ya watu waliouawa pamoja na jinai zilizofanyika katika vita hivyo ni kubwa na za kinyama zaidi kuliko zile zilizofanywa na utawala wa Saddam.
Mwaka 2003, serikali ya Marekani ikiongozwa na George Bush Jr ilitoa shutuma mbili dhidi ya serikali ya Iraq, moja ni kuwepo nchini humo silaha za kemikali za maangamizi ya umati na ya pili ni serikali ya Baghdad kuwa na uhusiano na magaidi wa al-Qaida; tuhuma mbili ambazo hazijathibitishwa hadi leo.
Kuhusu madai ya uwepo wa silaha za maangamizi ya umati nchini Iraq wananchi wa Marekani na Uingereza walikuwa na shaka kubwa kuhusu madai hayo kadiri kwamba walifanya maandamano ya kupinga vita dhidi ya nchi hiyo. Upinzani huo ulionekana wazi hata katika filamu na maandishi ya baadhi ya vyombo vya habari vya nchi mbili hizo za Magharibi. Upinzani huo uliongezeka hasa baada ya maafisa wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA kufanya uchunguzi wao wa kina nchini Iraq na kutangaza rasmi kwamba hawakuweza kupata silaha zozote za maangamizi ya umati katika ardhi ya nchi hiyo, kama ilivyokuwa ikidaiwa na Marekani na Uingereza.
Bila shaka, ikumbukwe kwamba wakati wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, Saddam aliwahi kutumia silaha za kemikali mara nyingi dhidi ya watu wa Iraq na raia wa Iran, lakini hakukabiliwa na hatua yoyote kutoka nchi za Magharibi kwa sababu zenyewe ndizo zilikuwa chanzo kikuu cha silaha hizo. La muhimu ni kuwa katika kipindi cha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iraq Marekani ilikuwa inatafuta kisingizio kizuri cha kuishambulia nchi hiyo na hakukuwepo na kisingizio kingine kizuri ghairi ya kuuhadaa ulimwengu kuwa ilikuwa inamiliki silaha za maangamizi ya umati na pia kuwa ilikuwa na uhusiano na magaidi wa al-Qaida.
Kuna uhusiano mkubwa kati ya mafuta na shambulio la Marekani dhidi ya Iraqi kutokana na mafuta kuwa suala la kimkakati kwa Marekani kwa ajili ya kudumisha nafasi yake kama nguvu kubwa duniani. Ingawa Jenerali Tommy Franks, kamanda wa operesheni ya uvamizi dhidi ya Iraq, alidai kuwa uvamizi huo ulifanyika kwa ajili ya kuwarejeshea Wairaqi mapato ya viwanda na visima vya mafuta, lakini mara tu baada ya Marekani kuung'oa madarakani utawala wa Saddam, iliyapa makampuni yake kandarasi za kusimamia shughuli za uendeshaji na usalama wa visima na viwanda vya nchi hiyo, makampuni ya kihalifu kama "Blackwater", ambalo baadaye lilitekeleza mauaji ya kutisha ya raia wa Iraq katika uwanja wa an-Nisour.
Jarida la "National Geographic" lilitangaza mnamo 2013, miaka 10 baada ya kuanza vita kwamba kutokana na uvamizi wa Marekani, Wairaqi milioni moja na laki moja walikimbia makazi yao na kwenda kuishi kambini, lakini Shirika la Msalaba Mwekundu lilikadiria idadi ya wakimbizi hao kuwa milioni mbili na laki tatu. Mnamo 2015, idadi hiyo ilifikia watu milioni nne na laki nne. Hayo yakiwa ni matokeo ya operesheni iliyodaiwa kuwa ni ya "kuwakomboa watu wa Iraqi"! Katika miaka 3 ya kwanza ya uvamizi wa Marekani zaidi ya nusu ya madaktari wa Iraqi walikimbia nchi. Kufikia 2007, utapiamlo wa watoto ulifikia asilimia 28. Ripoti rasmi zilionyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watoto wa Iraqi walikuwa wanakabiliwa na matatizo ya kiakili na kisaikolojia.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na taasisi na mashirika ya kimataifa ya utafiti, hasara ya kiuchumi iliyosababishwa na uvamizi huo ikiwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya viwanda, kilimo na afya, magonjwa yaliyosababishwa na maji yasiyofaa kwa matumizi, matumizi ya silaha zilizopigwa marufuku, hasa katika mkoa wa Basra, na uhalifu mwingine wa aina hiyo, inafikia dola bilioni 25.
Uharibifu mwingine usiosahaulika wa serikali ya Marekani dhidi ya taifa la Iraqi ni uundaji wa kundi la kigaidi la Daesh katika ardhi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa Donald Trump, serikali ya Marekani ndiyo ilikuwa muundaji mkuu wa kundi hilo la kigaidi na imekuwa ikitoa mafunzo kwa wanachama wake kwa muda mrefu. Kwa upande mwingine, hali ya ukosefu wa usalama ambayo ni matokeo ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq iliandaa mazingira mazuri ya kuimarishwa shughuli za kundi hilo la kigaidi. Uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Daesh dhidi ya miundombinu ya Iraq na magendo ya mafuta na wizi wa dhahabu ya nchi hiyo uliofanywa na kundi hilo inakadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 300. Katika uwanja wa kilimo pekee, Daesh iliharibu kabisa asilimia 40 ya kilimo cha Iraq.
Kwa mujibu wa takwimu hizi, ni wazi kabisa kwamba Marekani ilifanya jinai za kivita dhidi ya binadamu katika uvamizi wake wa kijeshi nchini Iraq, na inashangaza kuona mtu kama John Kerry, ambaye mwenyewe amesomea sheria, akificha ukweli huu usio na chembe ya shaka.