Jul 26, 2023 02:39 UTC
  • Jumatano, tarehe 26 Julai, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 8 Muharram 1445 Hijria, sawa na 26 Julai mwaka 2023.

Tarehe 8 Muharram mwaka 61 Hijria maji yaliadimika kabisa katika mahema ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala. Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kwamba: Katika siku ya nane ya Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena. Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe kamanda wa jeshi la Yazid mal'uuni, Umar bin Sa'd akimwambia: Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake." 

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Liberia ilipata uhuru. Liberia iko katika mwambao wa bahari ya Atlantic na inapakana na nchi za Guinea, Sierra Leone na Ivory Coast. Idadi kubwa ya raia wa nchi hiyo yenye jumla ya watu milioni tatu wanafuata dini za kijadi na kimila na asilimia 16 ya raia wake inaundwa na Waislamu. Lugha rasmi ya raia wa Liberia ni Kingereza. Liberia iliundwa mwaka 1822 kwa ajili ya Waafrika waliokuwa watumwa huko Marekani. Mwaka 1841 nchi hiyo iliandika katiba na kupewa jina la Liberia lenye maana ya ardhi ya watu huru.

Bendera ya Liberia

Miaka 167 iliyopita katika siku kama ya leo George Bernard Shaw mwandishi, muigizaji wa michezo ya kuchekesha na mkosoaji wa Ki-Ireland alizaliwa katika mji wa Dublin. Baba yake alikuwa mtumishi wa serikali. Akiwa katika rika la kuinukia George Bernard alianza kuandika visa na tamthiliya. Alijitihidi kutoa taswira ya matatizo ya kijamii katika visa vyake. 1925 Shaw alitunukiwa tuzo ya nobel ya fasihi.   

George Bernard Shaw

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, Reza Pahlavi maarufu kwa jina la Rezakhan mwasisi wa silsila ya Pahlavi nchini Iran alifariki dunia nchini Afrika Kusini baada ya kukalia kiti cha usultani kwa miaka 16 na kuwa uhamishoni kwa miaka mitatu. Rezakhan alizaliwa mwaka 1257 Hijria Shamsiya sawa na mwaka 1878, katika mojawapo ya vijiji vya kaskazini mwa Iran. Mwaka 1299 Hijria Shamsiya, sawa na mwaka 1920, Miladia Rezakhan alipewa amri na Uingereza ya kufanya mapinduzi nchini Iran ili kulinda maslahi ya serikali ya London, wakati alipokuwa afisa wa jeshi la Iran. Baadaye akawa Waziri wa Ulinzi na kisha Waziri Mkuu. Hatimaye mwaka 1304 Hijria Shamsiya sawa na mwaka 1925, Rezakhan alianzisha utawala wa silsila ya Qajar na kukalia kiti cha usultani nchini Iran licha ya kupingwa na wanazuoni na wanasiasa wapigania uhuru. 

Mwili wa Rezakhan 

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, Gamal Abdul-Nasser rais wa wakati huo wa Misri alitangaza kuutaifisha Mfereji wa Suez. Mfereji huo ulianzishwa mwaka 1896 baada ya Misri kukaliwa kwa mabavu na Uingereza na kwa utaratibu huo, njia ya baharini baina ya Ulaya na Asia ikawa imefupishwa. Udhibiti wa Uingereza na Ufaransa kwa Mfereji wa Suez uliendelea hadi serikali ya Abdu l-Nasser ilipokuja kuutaifisha na kuutangaza kuwa mali ya taifa. Hatua hiyo ilifuatiwa na mashambulio ya kijeshi ya Uingereza, Ufaransa na utawala dhalimu wa Israel. Hata hivyo mashinikizo ya kimataifa dhidi ya madola vamizi na mapambano ya wananchi Waislamu wa Misri, yalivifanya vikosi vamizi viondoke katika mfereji huo muhimu na ukawa katika miliki ya serikali na taifa la Misri. 

Gamal Abdul-Nasser

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita visiwa vya Maldives huko kusini mwa bara Asia vilipata uhuru. Visiwa vya Maldives vilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wareno mwanzoni mwa karne ya 16. Visiwa hivyo baadaye vilidhibitiwa na Waholanzi na Wafaransa na hatimaye mwishoni mwa karne ya 19, vikakaliwa na Waingereza. 

Bendera Maldives

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, yaani tarehe 26 Julai mwaka 1979,  Zuheir Mohsen Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya as-Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad) huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Magaidi wa Kizayuni walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo na polisi wa Ufaransa walidai kuwa hawakupata uthibitisho kwamba Mossad ilihusika na mauaji hayo.   

Zuheir Mohsen

Na miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, kiwanda kikubwa zaidi cha kusafishia mafuta mazito ya matumizi ya vyombo vya moto kilifunguliwa katika mji wa Bandar Abbas kusini mwa Iran. Kiwanda hicho kikubwa zaidi cha aina hiyo duniani kilitengenezwa na wataalamu wa Iran. Kiwanda hicho ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi na muhimu ya mafuta nchini Iran. 

Kiwanda cha kusafishia mafuta mazito, Bandar Abbas

 

Tags