Sura ya At-T’uur, aya ya 22-31 (Darsa ya 962)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 961 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 52 ya At-T’uur. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 22 hadi 24 ambazo zinasema:
وَأَمْدَدْنَاهُم بِفَاكِهَةٍ وَلَحْمٍ مِّمَّا يَشْتَهُونَ
Na tutawapa matunda, na nyama kama watavyopenda
يَتَنَازَعُونَ فِيهَا كَأْسًا لَّا لَغْوٌ فِيهَا وَلَا تَأْثِيمٌ
Watapeana humo bilauri zisizo na (vinywaji) vya kuleta maneno ya upuuzi wala dhambi.
وَيَطُوفُ عَلَيْهِمْ غِلْمَانٌ لَّهُمْ كَأَنَّهُمْ لُؤْلُؤٌ مَّكْنُونٌ
Iwe wanawapitia watumishi wao kama kwamba ni lulu zilizomo katika chaza.
Katika darsa iliyopita zilizungumziwa neema watakazopata watu wa Peponi. Aya hizi tulizosoma zinaashiria baadhi ya neema za vyakula na vinywaji na kueleza kwamba: kila aina ya matunda wataandaliwa watu wa Peponi, na aina yoyote ile ya matunda hayo watakayotamani watu hao watapatiwa papo hapo, kinyume na ilivyo hapa duniani, ambapo kila matunda huwa na msimu wake maalumu au huweza kupandwa yakaota katika eneo makhsusi la kijiografia. Lakini mbali na anuai za matunda, kwa upande wa aina mbalimbali za proteini za nyama, kuanzia ndege warukao angani, samaki wa baharini mpaka nyama hoa wa majangwani, nyama yoyote ile kati ya hizo watakayotamani watu wa Peponi watapatiwa bila ya mpaka wala kizuizi chochote. Ni kawaida kwamba, palipo na chakula kinahitajika na kinywaji pia. Huko Peponi kutakuwa na mvinyo, ambao watu wa humo watapeana na kunywa, na ladha yake itawapa raha isio na kifani pasi na kuwasababishia ubaya wala madhara yoyote iliyonayo pombe na ulevi wa hapa duniani, unaomlewesha na kumropokesha mtu maneno yasiyoeleweka, bali hata kumtumbukiza kwenye lindi la madhambi na vitendo vibaya na viovu. Watumishi na wahudumu jamili na wazuri wa Peponi, nao pia watakuwa tayari muda wote kuwahudumia watu wa humo kwa kuwaandalia kila wakitakacho ili wasijihisi wamepungukiwa na chochote kile zinachokitamani nafsi zao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, vyakula na vinywaji vya Peponi ni vingi bila idadi na vya aina mbalimbali; na vinaendana na hamu na matakwa ya wakazi wa humo ili wale na wanywe pasi na kuwasababishia maumivu wala kuchoshwa na kukinaishwa navyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wale ambao hapa duniani wanajiepusha na maovu na mambo ya upuuzi, makazi yao huko Akhera yatakuwa ni Peponi, mahali ambapo wanstahiki kuishi watu wenye sifa hizo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mvinyo wa Peponi hausababishi madhara kama ulivyo ule wa duniani. Haumleweshi mtu na kumfanya aropokwe maneno ya ovyo na ya kipuuzi, wala kufanya mambo maovu na yasiyostahiki.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 25 hadi ya 28 ambazo zinasema:
وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ
Wataelekeana wakiulizana.
قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ
(Waseme): Tulikuwa zamani tukiwaogopea (kwa kuwatakia kheri) ahali zetu.
فَمَنَّ اللَّهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ
Basi Mwenyezi Mungu ametufanyia ihsani na akatulinda na adhabu ya (Moto) unaounguza.
إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلُ نَدْعُوهُ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ
Hakika sisi zamani tulikuwa tukimwomba Yeye tu. Hakika Yeye ndiye Mwema Mwenye kurehemu.
Aya hizi zinasimulia mazungumzo na maulizano yatakayojiri baina ya watu wa Peponi na kueleza kwamba: baadhi ya maulizano hayo yatahusu yale yaliyowatokezea huko nyuma hapa duniani, kwamba walifanya mema gani mpaka Allah SWT akawaneemesha wao neema hiyo isiyo na kifani ya Pepo. Jawabu muhimu zaidi itakayotolewa kwa suali hilo ni kuhusu namna walivyokuwa wakizihofia, wakizihurumia na kuchelea hali ya familia na ahali zao. Watu hao walitekeleza kwa usahihi jukumu lao kwa wazazi wao, waume au wake zao pamoja na watoto wao na wakafanya kila waliloweza ili watu wao hao wasije wakaiacha na kuikengeuka njia ya haki. Hawakujilinda na kujiepusha wao wenyewe tu na madhambi, lakini walijitahi sana pia kuwapa malezi watoto wao ili wawe watu wema na waumini. Ni wazi kwamba, jitihada na huruma kama hizo hazikosi rehma za Allah; na kutokana na rehma hizo, jamaa wa familia zao watakuwa pamoja nao Peponi na wao wote Mola Mrehemevu atawanusuru na adhabu ya Moto. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, Pepo na Moto vinatokana na sisi wenyewe. Amali na mtendo yetu ya hapa duniani ndiyo yatakayotukutanisha Siku ya Kiyama na moja kati ya hatima mbili hizo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, dukuduku, kuifikiria na kuionea uchungu familia, kunakomfanya mtu awape watoto wake malezi sahihi ndio ufunguo wa Peponi. Kuwa na sifa hii ndiko kunakompelekea mtu mwenyewe na watoto wake wawe watu wa Peponi, -Allah atujaalie kuwa miongoni mwao-. Halikadhalika aya hizi zinatuonyesha kuwa, wanavyoamini watu wa Peponi, wao kuipata Pepo kunatokana na rehma za ihsani ya Mwenyezi Mungu, na si kwamba neema hiyo itakuwa ni malipo ya amali zao chache walizofanya hapa duniani; kwani amali hizo haziwezi kulinganishwa hata chembe na neema zisizo na ukomo za Peponi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 29 hadi 31 za sura yetu ya At-T'uur ambazo zinasema:
فَذَكِّرْ فَمَا أَنتَ بِنِعْمَتِ رَبِّكَ بِكَاهِنٍ وَلَا مَجْنُونٍ
Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu.
أَمْ يَقُولُونَ شَاعِرٌ نَّتَرَبَّصُ بِهِ رَيْبَ الْمَنُونِ
Au wanasema: Ni mshairi, tunamtazamia kupatwa na mauti.
قُلْ تَرَبَّصُوا فَإِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُتَرَبِّصِينَ
Sema: Ngojeeni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika wangojeao.
Baada ya kutajwa neema za Peponi katika aya zilizotangulia, katika aya tulizosoma, Allah SWT anamhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba: endelea kila mara kuwatanabahisha watu mambo haya na kuwakumbusha juu ya Kiyama ili kushughulishwa kwao na maisha ya dunia kusije kukawasahaulisha akhera. Kwa kupewa ukumbusho juu ya mambo hayo, washirikina kwa upande wao, walimwita Bwana Mtume Muhammad SAW kuhani na kusema, yeye kama walivyo makuhani wote anafanya uaguzi kuhusu yatakayojiri siku za usoni, anazungumzia mustakabali na kutaka kuwaelewesha watu siri za mambo ya ghaibu. Na ndio maana anawasiliana na majini na kupokea kutoka kwao habari za siku za usoni. Mwenyezi Mungu Mtukufu akawajibu washirikina hao kwa kuwaambia: Mtume kujua yatakayojiri siku za usoni kunatokana na Wahyi anaoteremshiwa na kwa sababu ya Utume na ujumbe anaolingania. Yeye hafanyi ukuhani wala hana mawasiliano na majini, kama ambavyo si mtunzi wala si msanifu wa mashairi. Ayasemayo ni maneno ya Allah SWT, si fikra wala mambo anayowaza ndani ya nafsi yake, mkadhani kwamba akiondoka yeye, zama za mambo yake zitamalizika na nafasi yake kuchukuliwa na kuhani au mshairi mwingine. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wapinzani wa Mitume walikuwa siku zote wakijaribu kuwatenganisha watu na kuwaweka mbali na waja hao wateule, kwa kuwanasibisha na sifa mbaya wasizostahiki kama kuwaita washairi, makuhani na wendawazimu. Aidha aya hizi zinatuonyesha kuwa, maadui wa Uislamu walitarajia kwamba baada ya kutawafu na kuondoka duniani Bwana Mtume SAW nuru ya Uislamu itazimika, lakini irada ya Allah SWT imeshapitisha kuwa nuru hiyo iendelee kuangaza daima na kung'ara kwa nguvu kubwa. Ni kama tuonavyo leo hii, ambacho licha ya njama na uadui wote unaofanyiwa, Uislamu unazidi kuenea na kukubaliwa duniani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 962 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe ushujaa na uthabiti wa kuinusuru dini yetu, atujaze nyoyoni mwetu mapenzi ya Mtume wetu na atupe ujasiri na ghera ya kukitetea Kitabu chetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/