Oct 11, 2023 06:38 UTC
  • Sura ya Al-Qamar, aya ya 43-55 (Darsa ya 973)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 973 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 54 ya Al-Qamar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 43 hadi ya 46 ya sura hiyo ambazo zinasema:

أَكُفَّارُكُمْ خَيْرٌ مِّنْ أُولَٰئِكُمْ أَمْ لَكُم بَرَاءَةٌ فِي الزُّبُرِ

Je! Makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani?

أَمْ يَقُولُونَ نَحْنُ جَمِيعٌ مُّنتَصِرٌ

Au ndio wanasema: Sisi ni wengi tutashinda tu.

سَيُهْزَمُ الْجَمْعُ وَيُوَلُّونَ الدُّبُرَ

Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma. 

بَلِ السَّاعَةُ مَوْعِدُهُمْ وَالسَّاعَةُ أَدْهَىٰ وَأَمَرُّ

Bali Saa ya Kiyama ndio miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi.

Tangu tulipoianza tarjumi na maelezo ya Suratul-Qamar hadi sasa, zimezungumziwa hatima chungu na mbaya zilizowapata watu wa kaumu zilizoasi na kuikadhibisha haki. Aya hizi tulizosoma zinawahutubu washirikina wa Makka kwa kuwahoji: kwa nini nyinyi hamupati ibra na mazingatio mkaacha kuabudu masanamu na amali hizo ovu na mbaya mnazofanya? Kwani mnajidhani kwamba nyinyi ni bora kuliko watu hao? Au mnahisi kwamba ukafiri na kuasi kwenu nyinyi ni kudogo kulinganisha na wao na kwa hivyo haitakufikeni adhabu ya Mwenyezi Mungu? Au mumeletewa barua itokayo kwa Mwenyezi Mungu kwamba nyinyi mtakuwa katika salama na mumesamehewa kufikwa na adhabu? Huenda mnadhani pia kwamba nguvu zenu ni kubwa kiasi ambacho hakuna yeyote mwenye uwezo wa kukabiliana na nyinyi, na nyinyi mnaweza kupingana na irada ya Allah SWT? Hali ya kuwa akitaka Yeye Allah, hata hili kundi dogo tu la Waislamu litaweza kukushindeni kwa kuusambaratisha umati wenu mkatimua mbio katika medani ya vita. Hiyo itakuwa hatima yenu ya hapa duniani, na kwa yakini adhabu itakayokufikeni Siku ya Kiyama itakuwa nzito zaidi na yenye kuumiza zaidi pia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kujikweza na kujivuna kunaweza kuwa sababu ya kumporomosha na kumuangamiza mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tusitegemee sana nguvu na suhula tulizonazo wala msaada na uungaji mkono wa watu wengine; badala yake tutawakali na kutegemea nguvu na uwezo mutlaki na usio na kikomo wa Allah SWT na kuacha kuhadaiwa na kiburi na ghururi zisizo na msingi. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kushindwa kwa dhulma na ukafiri ni ahadi ya uhakika ya Allah na isiyo na chembe ya shaka; na nguvu na uwezo walionao makafiri na madhalimu havitazuia wao kudhoofika na kuangamia.

 

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 47 hadi ya 50 ya sura hii ya Al-Qamar ambazo zinasema:

إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ

Hakika waovu wamo katika upotofu na moto.

يَوْمَ يُسْحَبُونَ فِي النَّارِ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ ذُوقُوا مَسَّ سَقَرَ

Siku watakapo kokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: Onjeni mguso wa Jahannamu!

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo. 

وَمَا أَمْرُنَا إِلَّا وَاحِدَةٌ كَلَمْحٍ بِالْبَصَرِ

Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.

Katika aya zilizotangulia imezungumziwa adhabu itakayowafika waovu hapa duniani. Aya hizi tulizosoma zinaashiria adhabu kali itakayowapata Siku ya Kiyama na kueleza kwamba, walipokuwa duniani, badala ya watu hao kuchagua njia sahihi, walifuata njia pogo na za upotofu. Kwa kufanya hivyo, walijitafutia wenyewe sababu za kupotoka; na matokeo yake ni kwamba, kuasi na kufanya madhambi ikawa ndio njia na mwenendo wao katika maisha yao yote. Ni wazi kwamba, Siku ya Kiyama hawatakuwa tayari kuingia motoni kwa hiari yao; kwa hivyo Malaika wa adhabu watawasukumiza Motoni kifudifudi kwa nyuso zao ili waweze kuuhisi barabara muunguzo wa Jahanamu ndani ya nafsi zao na ujudi wao wote kutokana na yale waliyokuwa wakiyakanusha na kuyakadhibisha duniani. Pamoja na hayo, Siku ya Kiyama, baadhi ya watu watahoji, kutokana na kuhisi kwamba hakuna mlingano baina ya dhambi walizofanya duniani na adhabu kali itakayowafika siku hiyo. Katika sehemu inayofuatia ya aya tulizosoma, shubha na utata huo unatolewa jibu, nalo ni la kwamba, kama ambavyo mfumo wa uumbaji umewekewa kipimo na kiwango maalumu, mfumo wa utoaji malipo ya thawabu na adhabu pia umewekewa hesabu na makadirio yake makini na maalumu; kwa hiyo hukumu inayotolewa na Allah juu ya mambo hayo haina hata chembe ya dhulma na uonevu, japokuwa kutokana na ujuzi mdogo wa mambo na wenye ukomo alionao mwanadamu, unaweza ukamfanya apitikiwe na suali na utata kama huo. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, tuchunguze na tuwe makini katika kuchagua njia ya maisha ili tuweze kufika tulikokusudiwa. Vyenginevyo, tutapotea njia na kuishia kwenye ubabaikaji na hali ya kutangatanga. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama ambavyo mbingu na ardhi zimeumbwa na Allah katika dunia hii na kila kimoja kimewekewa hesabu, vipimo na makadirio maalumu, katika ulimwengu wa akhera pia Pepo na Moto, navyo pia vitawekwa kwa msingi wa haki na uadilifu na mfumo wa utoaji malipo ya thawabu au adhabu utafuta utaratibu na mahesabu maalumu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 51 hadi 55 ya sura yetu ya Al-Qamar ambazo zinasema:

وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا أَشْيَاعَكُمْ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ

Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Basi je, yupo anaye kumbuka? 

وَكُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ

Na kila jambo walilo lifanya limo vitabuni. 

وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُّسْتَطَرٌ

Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa. 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَهَرٍ

Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito.

فِي مَقْعَدِ صِدْقٍ عِندَ مَلِيكٍ مُّقْتَدِرٍ

Katika makao ya kweli kwa Mfalme Mwenye uweza. 

Aya hizi, ambazo ni aya za mwisho za Suratul-Qamar ni onyo kwa watu wabaya na bishara kwa waja wema; lakini pia zinawataka wote hao wapate funzo, ibra na mazingatio kutokana na hatima iliyozipata kaumu zilizopita, ambazo zilikuwa za watu wanaofanana na nyinyi; na mjue kwamba hakuna tendo au amali yoyote ile iwezayo kufichika mbele ya elimu na ujuzi wa Allah na kila jema na baya mlifanyalo linasajiliwa na kuhifadhiwa kwenye madaftari ya amali zenu. Tambueni pia kuwa Siku ya Kiyama, mfumo wa utoaji malipo ya thawabu na adhabu utakuwa na umakini wa hali ya juu kabisa na utatekelezwa kwa kutegemea ushahidi uliosajiliwa. Amali za waja wema, kwa kuwa walizifanya kwa ikhlasi, tena mbali na macho ya watu na hakukuwa na yeyote aliyekuwa na taarifa nazo ghairi ya Allah SWT, zitalipwa malipo kamili ya thawabu. Hadhi na daraja aali watakayowekwa waja safi na wema ni maalumu na ya aina ya pekee; daraja na hadhi ambayo haiwezi kueleweka na kufahamika kwa watu wa ulimwengu huu tunaoishi. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, mfumo wa Allah wa utoaji malipo ya thawabu na adhabu ni wa haki na uadilifu; na watu wa kaumu zote watalipwa namna moja, kama ni thawabu au adhabu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, japokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi wa kila kitu na Yeye mwenyewe ndiye mmiliki na hakimu wa Siku ya Malipo, lakini pamoja na hayo, matendo na amali zote za wanadamu, kubwa na ndogo zinasajiliwa na malaika na kuhifadhiwa kwa nidhamu na umakini wa juu kwenye madaftari maalumu ili kisipatikane kisingizio cha aina yoyote kwa mtu kukanusha lolote lile. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, malipo ya thawabu ya watu wa peponi si ya vitu vya kimaada na kimwili pekee. Kuhudhurishwa mbele ya hadhara tukufu ya Allah Jalla fii U'laahu na kupata neema ya kuwa pamoja na manabii, mawalii na waja wema wa duniani ni miongoni mwa fadhila na neema za kimaanawi walizoandaliwa waja wema wa Peponi, ambazo raha na utamu wake hauwezi kuelezeka, -Allah atujaalie kuwa miongoni mwa watakaoruzukiwa neema hizo-, amin. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 973 ya Qur'ani imefikia tamati, na ndiyo inayotuhitimishia tarjumi na maelezo ya sura ya 54 ya Al-Qamar. InshaaLlah tuwe tumenufaika na kuaidhika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atupokelee mema yetu, aufanye mwema mwisho wetu na aijaalie Pepo yake ya milele yawe ndio makazi yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags