Oct 11, 2023 10:47 UTC
  • Sura ya Ar-Rahman, aya ya 1-9 (Darsa ya 974)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 974. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 54 ya Al-Qamar, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa ufupi ya sura ya 55 ya Ar-Rahman. Sura hii imeanza na neno "Ar-Rahman", ambalo ni moja ya majina na sifa za Mwenyezi Mungu Mtukufu inayobainisha rehma nyingi na zisizo za ukomo za Allah SWT katika mfumo wa uumbaji. Katika sura hii, ambayo ina jumla ya aya 78, zimetajwa aina kwa aina za neema za vitu vya kimaada na za kimaanawi na kiroho za Allah SWT za hapa duniani na huko akhera; na baada ya kubainishwa kila neema, wanaulizwa waja wa Mwenyezi Mungu, ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayoikanusha? Baada ya utangulizi huo mfupi, sasa tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya mwanzo hadi ya nne ya sura hiyo ambazo zinasema:

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa Jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

الرَّحْمَٰنُ

Ar-Rah'man, Mwingi wa Rehema

عَلَّمَ الْقُرْآنَ

Amefundisha Qur'ani. 

خَلَقَ الْإِنسَانَ

Amemuumba mwanaadamu,

عَلَّمَهُ الْبَيَانَ

Akamfundisha ubainifu.

Jina la Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'ani ni Allah; na Ar-Rahman ni moja ya sifa zake Yeye Mola. Lakini sifa hii inabainisha rehma nyingi mno za Allah zilizokienea kila kitu, mpaka limetumika kumtaja Mwenyezi Mungu kama lilivyo jina Allah, na hivyo kuwa jina lake Mola, kama lilivyotumika katika sura hii badala ya jina Allah. Kuteremshwa Qur'ani na kufundishwa Bwana Mtume Muhammad SAW na kisha wakafundishwa wanadamu wote na majini, ni jambo lenye thamani kubwa, kiasi kwamba ndani ya sura hii ya Ar-Rahman, suala hilo limetangulizwa kabla ya suala la asili zaidi la kuumbwa mwanadamu. Naam, ukweli ni kwamba thamani ya mtu inapatikana pale anapopiga hatua kwenye njia ya uongofu na kufuata njia iliyo sahihi. Kati ya sifa kadhaa za mwanadamu, aya tulizosoma zimegusia uwezo wa kutamka na kuzungumza, jambo ambalo linampambanua kiumbe huyo na wanyama; kwa sababu wanyama, nao pia kama alivyo mwanadamu, wana macho na masikio; lakini uwezo huu wa utamkaji maneno na uzungumzaji ni katika sifa maalumu za upendeleo alizojaaliwa mwanadamu. Ifahamike pia kwamba, ubainifu, ambao katika maana yake pana unajumuisha pia herufi na uandishi, una nafasi muhimu katika mageuzi na kupiga hatua maisha ya wanadamu na kujitokeza na kustawi kwa tamaduni mbalimbali. Lau kama mwanadamu asingejaaliwa neema hiyo ya ubainifu asingeliweza katu kurithisha na kupokeza elimu na tajiriba zake kutoka kizazi kimoja hadi kingine; na matokeo yake ni kwamba yasingepatikana mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya elimu, sayansi na teknolojia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, sifa pana na jumuishi zaidi ya Allah SWT, ambayo inajumuisha viumbe wote na ndio asili na chimbuko la mfumo wa uumbaji na upangaji sheria ni sifa ya rehma. Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaka jambo lolote linalofanywa lianzwe kwa kutamka "Bismillahi Rahamani Rahim" ili kila mara tunapotaja jina lake tukufu ziashiriwe pia rehma zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ufundishaji ni mojawapo ya mambo yafanywayo na Allah SWT. Ukweli ni kwamba mwalimu wa mwanzo wa mwanadamu ni Mwenyezi Mungu; na rehma, ni jambo linalohitajika katika ufunzaji na ufundishaji. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuumbwa kwa mwanadamu akiwa na sifa za kuweza kufunzika, kuelimika na kutaalamika ni dhihirisho mojawapo la rehma za Mwenyezi Mungu, kama ambavyo kufundishwa Qur'ani kwa ajili ya uongofu wa wanadamu ni dhihirisho jingine la rehma hizo. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, uwezo wa ubainifu ambao nao pia ni wenzo wa kufikishia elimu na tajiriba kwa wanadamu ni miongoni mwa rehma za Mwenyezi Mungu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya tano na ya sita ya sura yetu ya Ar-Rahman ambazo zinasema:

الشَّمْسُ وَالْقَمَرُ بِحُسْبَانٍ

Jua na mwezi huenda kwa hisabu.

وَالنَّجْمُ وَالشَّجَرُ يَسْجُدَانِ

Na mimea na miti, inasujudu. 

Baada ya kutajwa neema ya kuteremshwa Qur'ani na uwezo wa ubainifu ambayo ni miongoni mwa sifa zinazompambanua mwanadamu kwa kumtafautisha na viumbe wengine, aya hizi tulizosoma, kwanza zinaangazia ulimwengu wa mbinguni na kisha wa ardhini na kueleza kwamba, jua na mwezi vimo kwenye mwendo unaofuata nidhamu makhsusi, kwa hisabu makini na utaratibu maalumu. Kiwango cha uzito na ukubwa wa kila moja kati ya maumbo hayo, masafa yaliyopo baina yao na baina ya viwili hivyo na sayari ya dunia, yote hayo yamewekewa makadirio na hesabu maalumu, kiasi kwamba, kwa mfano, kama masafa kutoka sayari ya dunia hadi lilipo jua yataongezeka au kupungua, wanadamu wote na viumbe vingine hai vilivyoko ardhini vitaangamia kutokana na baridi kali au joto kali kupindukia. Mzunguko wa sayari ya dunia kujizunguka yenyewe unaopelekea kupatikana usiku na mchana, na vilevile mzunguko wake wenye nidhamu na mahesabu maalumu wa kulizunguka jua unaopelekea kupatikana miezi na misimu tofauti ya mwaka na halikadhalika mzunguko wa mwezi kuizunguka dunia kupitia mzingo wake maalumu, vyote hivyo ni mifano dhahiri na ya wazi kabisa ya kuwepo nidhamu na mahesabu makini yanayotawala katika ulimwengu wa maumbile. Kwa mtazamo wa wanasayansi, mzunguko wa mwezi na jua katika mizingo yao unafanyika kwa mpangilio na nidhamu makini, kiasi cha kuwawezesha wao kutambua kwa makumi ya miaka kabla, ni siku gani na katika saa na dakika ngapi, kupatwa kwa mwezi na jua kutatokea. Nukta nyingine ni kwamba, kuwepo kwa jua, -sayari hiyo yenye joto na muunguzo mkali wa moto-, ni miongoni mwa neema kubwa kabisa kwa wanadamu, kwa sababu bila mwangaza wake na joto lake, maisha yasingewezekana kwa viumbe wa ardhini. Uchipuaji na ukuaji wa mimea na miti na mazao yake yanayohitajiwa kwa ajili ya chakula cha watu, unyeshaji wa mvua na uvumaji wa pepo, vyote hivyo vinapatikana kwa baraka za uwepo wa jua. Mwezi nao kwa upande wake, unatoa mchango muhimu katika maisha ya wanadamu. Katika usiku wa giza totoro, umbo hilo la angani hutoa mwangaza mithili ya taa. Nguvu yake ya uvutano, ambayo ndiyo chanzo cha kupatikana mawimbi ya bahari, ina mchango mkubwa kwa maisha ya viumbe wa baharini na hali ya mwingiliano wa chini ya ardhi. Kwa upande wa ardhini pia, kuna aina kwa aina za mimea na miti, ambayo ndiyo chanzo cha upatikanaji wa chakula kwa wanadamu na viumbe vyengine vyenye uhai. Vyote hivyo na wote hao wanafuata kanuni za kimaumbile alizowapangia Mwenyezi Mungu; na hakuna chochote kinachokengeuka hata chembe kanuni na taratibu hizo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mbingu na ardhi zinaendeshwa kwa kufuata mfumo makini na maalumu ziliowekewa; na hakuna hata kimoja kati ya viwili hivyo kinachokengeuka njia na mkondo huo uliowekwa na Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ulimwengu wa maumbile haujampunja mwanadamu chochote kile anachohitajia kwa ajili ya huduma na mahitaji yake, lakini yeye mwanadamu anaamiliana na maumbile kana kwamba nia na dhamira yake ni kuhakikisha anauangamiza ulimwengu wa maumbile na mazingira yake. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ulimwengu wote umejisalimisha kufuata nidhamu na utaratibu uliopangwa na kunadhimiwa tokea kabla na Allah SWT.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya saba hadi ya tisa ya sura yetu ya Ar-Rahman ambazo zinasema:

وَالسَّمَاءَ رَفَعَهَا وَوَضَعَ الْمِيزَانَ

Na mbingu ameziinua, na ameweka mizani,

أَلَّا تَطْغَوْا فِي الْمِيزَانِ

Ili msidhulumu katika mizani.

وَأَقِيمُوا الْوَزْنَ بِالْقِسْطِ وَلَا تُخْسِرُوا الْمِيزَانَ

Na wekeni mizani kwa haki, wala msipunje katika mizani.

Aya hizi zinaendeleza yale yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kuashiria uumbaji wa sayari na maumbo adhimu ya angani yanayojumuisha mabilioni ya nyota na sayari, ambayo yamewekewa na kupangiwa na Allah mfumo na mzingo maalumu wa kupitia na kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu ambaye ameziinua mbingu hizi zenye adhama kubwa, ameweka pia kipimo na mizani kwa ajili ya mfumo wa sharia, ili kwa sharia hizo muweze kuitambua haki na uadilifu na kujiweka mbali na batili. Tumieni mizani ya haki na batili katika masuala ya mali na uchumi, ya haki za mtu binafsi na jamii na jiepusheni na kufurutu mpaka katika kutekeleza haki za watu; na haki na uadilifu viwe daima ndio kipimo mnachotumia katika kuamiliana na watu. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, mfumo wa ulimwengu umesimamishwa juu ya msingi wa mizani na nidhamu makini; na si kwamba umejitokeza kwa sadfa na bahati tu bila ya kuwekewa mpango na utaratibu tokea hapo kabla. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama ilivyo kwa ulimwengu wa maumbile ambao umeumbwa kwa kuwekewa mizani na nidhamu maalumu, uteremshwaji wa wahyi pia umefanywa kwa nidhamu na utaratibu huohuo ili watu wahakikishe katika mambo yao wanachunga na kuzingatia haki na uadilifu kwa kutumia mizani ya akili waliyojaaliwa na wahyi walioteremshiwa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 974 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags