Nov 15, 2023 10:26 UTC
  • Sura ya Ar-Rahman, aya ya 10-18 (Darsa ya 975)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 975 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 55 ya Ar-Rahman. Tunaianza darsa yetu kwa aya yake ya 10 hadi ya 13 ambazo zinasema:

وَالْأَرْضَ وَضَعَهَا لِلْأَنَامِ

Na ardhi ameiweka kwa ajili ya viumbe.

 فِيهَا فَاكِهَةٌ وَالنَّخْلُ ذَاتُ الْأَكْمَامِ

Humo yamo matunda na mitende yenye mafumba. 

وَالْحَبُّ ذُو الْعَصْفِ وَالرَّيْحَانُ

Na nafaka zenye makapi, na miti yenye harufu nzuri. 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ

Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha nyinyi wawili?

Kati ya neema za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu ni kumuandalia kiumbe huyo tandiko la ardhi la kuishi juu yake na kuendelea kubaki kizazi chake. Kwa mujibu wa ushahidi wa kibiolojia, viliwahi kuwepo viumbe hai vingi sana, ambavyo vimetoweka katika zama mbalimbali zilizopita au vinaendelea kutoweka hivi sasa pia. Lakini kizazi cha mwanadamu kimekuwa kikiongezeka daima na suhula zote zinazohitajika kukiwezesha kiendelee kubaki ardhini zinaendelea kupatikana. Moja ya vitu vinavyoendeleza maisha ya mwanadamu ni mimea na miti inayoota ardhini, pamoja na aina kwa aina za mazao na matunda yanayotokana na mimea na miti hiyo, ambayo yote hayo ni chakula kikuu kinacholiwa na mwanadamu. Vyakula hivyo vya mimea hukidhi mahitaji yote ya mtu na vinaendana na mfumo wake wa umengényaji na usagaji chakula. Wanyama pia, ambao nyama yao inatumiwa na mwanadamu, wanapata chakula chao kutoka kwenye mimea hiyohiyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuzitambua neema za Mwenyezi Mungu humwezesha mtu kupata ufahamu na uelewa wa kuutambua ujuzi, qudra, uwezo na rehma zake na hivyo kuonyesha khudhuu na unyenyekevu kwake Yeye Mola Muumba. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, matunda yanatoa mchango muhimu katika chakula cha mwanadamu; na kati ya matunda mbalimbali, tende tábán zina faida maalumu za lishe, na ndiyo maana zimeashiriwa kwa uzito makhsusi katika aya tulizosoma. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mimea yenye harufu nzuri na harufu ya manukato itokanayo na mimea hiyo ni neema nyingine ya Allah kwa wanadamu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 14 hadi 16 ya sura yetu ya Ar-Rahman ambazo zinasema:

خَلَقَ الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ كَالْفَخَّارِ

Amemuumba mtu kwa udongo mkavu kama uliookwa.

وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ

Na akawaumba majini kwa mwale wa moto. 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ 

Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha nyinyi wawili?

Aya hizi zinazungumzia uumbwaji wa mwanadamu na jini, wakiwa ni viumbe wenye hisi za ufahamu na uelewa, wanaoishi katika sayari ya dunia na kueleza kwamba, mwanadamu, ambaye ndiye mwanakindakindaki wa ulimwengu huu, ameumbwa kwa kitu duni na chenye thamani ndogo kabisa, yaani udongo, ambao baada ya kuchanganyika na maji hubadilika kuwa kitu kigumu katika sura na muundo wa vitu kama chungu na tofali. Kwa maana hiyo, thamani ya mwanadamu haitokani na kiwiliwili chake ambacho kimefinyangwa kwa udongo mkavu, bali inatokana na roho yake aliyopuliziwa na Allah SWT. Jini, naye pia ni mmoja wa viumbe wa Mwenyezi Mungu ambaye ametajwa katika aya kadhaa za Quráni tukufu; na hata kuna sura ndani ya Quráni iitwayo Suratul-Jin. Kwa mujibu wa aya tulizosoma, jini ametokana na moto; na kwa kutumia hoja hiyohiyo, shetani Iblisi ambaye ni miongoni mwa majini, alijinasibu na kujiona bora kuliko Adam AS, aliyeumbwa kwa udongo; hali ya kuwa hakuna hoja wala sababu yoyote inayoufanya moto uwe bora zaidi kuliko udongo na maji. Lakini mbali na hayo, si mwanadamu wala jini, ambaye amehusika kwa namna yoyote ile katika asili ya kuumbwa na kuwepo kwake. Ukweli ni kwamba majini na wanadamu, wanapaswa kuwa washukurivu kwa Mola wao, aliyewaumba na kuwapa uhai na kuwatunuku neema za aina kwa aina. Lakini kwa masikitiko ni kwamba akthari ya jamii za makundi yote hayo mawili ya viumbe ni watovu wa shukurani kwa Mola na Muumba wao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, maji, udongo na moto si vitu vyenye uhai; lakini Allah SWT ameumba kutokana na vitu hivyo, viumbe hai na wenye hisi na akili; na hii ni moja ya neema kubwa za Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, jini na mwanadamu, wote wawili ni viumbe wa ardhini na wameumbwa kutokana na kitu cha kimaada. Halikadhalika, aya hizi zinatuelimisha kwamba, tusikanushe na kukadhibisha tusichokiona na kilichofichikana mbele ya hisi zetu. Jini, neno ambalo maana yake ni kiumbe kisichoonekana, na ambaye sisi hatuwezi kumuona ni miongoni mwa viumbe wa Allah, na kuwepo kwake hakuwezi kukanushika. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kuwa, kukufuru neema ni jambo baya na linalokemewa; na wote wawili, mwanadamu na jini, wana sifa na mwenendo huu muovu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 17 na 18 za sura yetu ya Ar-Rahman ambazo zinasema:

رَبُّ الْمَشْرِقَيْنِ وَرَبُّ الْمَغْرِبَيْنِ

Mola Mlezi wa mashariki mbili na Mola Mlezi wa magharibi mbili. 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ 

Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayo ikanusha nyinyi wawili? 

Aya hizi zinamzindua tena mwanadamu azingatie mzingo wa mzunguko wa sayari ya dunia na kueleza kwamba, Mwenyezi Mungu, ambaye ameiumba ardhi na jua anaviendesha viwili hivyo kwa namna ambayo, wakati mwanga wa jua unapoangaza na kupiga ardhini hauwi na hali moja muda wote bali hubadilika ndani ya kipindi cha mwaka mzima. Unapoanza msimu wa joto kali jua huwa kwenye nukta ya juu kabisa angani na kutoa mwanga wenye joto la kiwango cha juu kabisa; na unapoanza msimu wa baridi kali, jua huwa kwenye nukta ya chini kabisa na kutoa mwanga wenye joto la kiwango cha chini zaidi kuangazia ardhini; na hali hiyo ndiyo inayopelekea kupatikana misimu minne ya mwaka. Nukta hizo mbili, kwa hakika ndizo mashariki mbili na magharibi mbili za kiwango cha juu na cha chini zaidi cha joto la jua na kwa hivyo mashariki na magharibi nyinginezo za ndani ya muda wote wa mwaka zinakuwepo baina ya mashariki na magharibi hizo mbili. Nukta nyingine ambayo inapasa tuiashirie hapa ni kwamba, jua, huwa kila siku katika masiku ya mwaka mzima linachomoza katika nukta moja na kuzama katika nukta nyingine; kwa hivyo lina idadi ya mashariki na magharibi kulingana na idadi ya siku za mwaka. Na ndio maana katika aya ya 40 ya Suratul-Maarij zimeashiriwa mashariki na magharibi kwa sura ya wingi ikimaanisha mashariki na magharibi tofauti za jua, kwenye kila moja ya siku za mwaka. Lakini kama tulivyotangulia kueleza, katika aya hii ya Suratu-Rahman zimeashiriwa mashariki mbili na magharibi mbili zilizopo katika kipindi cha mwaka mzima, huku mashariki na magharibi zingine zote zikiashiriwa kuwemo ndani ya mashariki na magharibi mbili hizo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Quráni, inamtolea mwito mwanadamu wa kuzitambua na kuzielewa mbingu na nyota. Kuzitambua neema za angani za Mwenyezi Mungu likiwemo jua, mwezi na nyota na mizingo ya kila moja kati ya maumbo hayo, ni jambo lililopewa umuhimu na mazingatio na Qur'ani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, siku kuwa fupi na ndefu na hewa kuwa ya joto na baridi katika vipindi tofauti vya mwaka si jambo linalotokea kwa sadfa na bahati tu, bali linatokana na tadbiri na uendeshaji mambo wa Allah na kwa kuzingatia mahitaji ya mzunguko wa maisha ya viumbe vyenye uhai vilivyoko ardhini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 975 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa washukurivu wa neema zake zote, kubwa na ndogo, tuzijuazo na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags