Sep 27, 2023 14:26 UTC
  • Sura ya Al-Qamar, aya ya 33-42 (Darsa ya 972)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 972 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 54 ya Al-Qamar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 33 hadi ya 35 ya sura hiyo ambazo zinasema:

كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ بِالنُّذُرِ

Watu wa Luti (pia) waliwakadhibisha Waonyaji.

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ حَاصِبًا إِلَّا آلَ لُوطٍ ۖ نَّجَّيْنَاهُم بِسَحَرٍ

Hakika Sisi tukawapelekea kimbunga cha vijiwe, isipo kuwa wafuasi wa Lut'i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri.

نِّعْمَةً مِّنْ عِندِنَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي مَن شَكَرَ

Kwa neema inayo toka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anaye shukuru.

Kaumu ya Lut ni kaumu ya nne iliyotajwa ndani ya sura hii ya Al-Qamar, ambayo nayo pia ilifikwa na hatima na mwisho mbaya kutokana na kuyapuuza maonyo ya Mtume wao. Mwenendo mchafu wa liwati na ujengaji mahusiano ya kingono baina ya mwanamme na mwanamme mwenzake ulikuwa umeenea na kuzoeleka kati ya wanaume wa kaumu hiyo, kiasi ambacho maonyo na indhari za mtawalia alizokuwa akiwapa Mtume wao kuhusu ubaya wa uovu huo na matokeo yatakayowapata, hazikuwa na taathira yoyote kwa watu hao. Badala ya kuyakubali maneno ya mantiki aliyokuwa akiwaambia Nabii Lut AS, watu wa kaumu hiyo walikwenda mbali zaidi kwa kumtishia kumfukuza Mtume huyo katika mji wao ili wapate kuepukana na nasaha alizokuwa akiwapa kwa uchungu na huruma. Mwenyezi Mungu aliwapelekea watu hao pia upepo mkali wa kimbunga ambao ulisomba wimbi kubwa la mchanga na changarawe na kulipeperusha angani kisha likawashukia ghafla na kwa mpigo watu waovu na mafasiki wa kaumu hiyo. Matokeo yake, nyumba na maskani za watu hao zilifunikwa na kuzikwa na zege hilo la kokoto na changarawe na wao wote wakaangamizwa. Lakini kabla ya kuteremshwa adhabu hiyo, Mwenyezi Mungu alimpa habari Mtume wake Lut AS kwa kumtaka yeye na watu wake, -ukiondoa mke wake ambaye alikuwa akishirikiana na watu hao waovu-, watoke nje ya mji ili wasalimike na adhabu ya Allah itakayowateremkia watu hao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutoa maonyo na indhari ni miongoni mwa majukumu yaliyokuwa yakitekelezwa na Mitume wote katika zama zote za historia, lakini akthari ya watu hawakuwa wakiyajali maonyo hayo wala kuaidhika kwa nasaha na indhari walizokuwa wakipewa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, uadilifu wa Allah unahukumu kwamba wakati wa kuteremshwa adhabu, inapasa waumini na waja wema waokoke na adhabu hiyo. Konde inapotaka kusafishwa, visiki na magugu ndivyo vinavyong'olewa vikachomwa moto na kutupwa, lakini miti na mimea yake yenye faida hutunzwa na kubakishwa. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba kuukubali wito wa Mitume na kufuata maamrisho ya wajumbe hao wa Allah ni aina mojawapo ya ushukurivu wa kivitendo, ambao hufuatiwa na malipo na neema za Mola hata hapa duniani pia.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 36 hadi 40 ya sura yetu hii ya Al-Qamar ambazo zinasema:

وَلَقَدْ أَنذَرَهُم بَطْشَتَنَا فَتَمَارَوْا بِالنُّذُرِ

Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo.

وَلَقَدْ رَاوَدُوهُ عَن ضَيْفِهِ فَطَمَسْنَا أَعْيُنَهُمْ فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ

Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: Onjeni basi adhabu na maonyo yangu! 

وَلَقَدْ صَبَّحَهُم بُكْرَةً عَذَابٌ مُّسْتَقِرٌّ

Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea.

فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ

Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ

Na hakika tumeifanya Qur'ani iwe nyepesi kuikumbuka. Basi je yupo anaye kumbuka?

Nabii Lut AS alikuwa akiwaonya na kuwatahadharisha kila mara watu wa kaumu yake juu ya hatima na mwisho mbaya utakaowafika kwa sababu ya vitendo vichafu na viovu walivyokuwa wakifanya, lakini watu hao walitilia shaka maneno yake na kuyaona hayaendani na ukweli. Lakini siku malaika wa Allah waliokuwa katika maumbo ya vijana wenye sura jamili walipofika nyumbani kwa Nabii Lut AS, baadhi ya wahuni na waovu waliofurutu mpaka katika maasi ya liwati, walimtaka Mtume wao huyo awapatie wao wageni wake hao. Kwa amri ya Allah, macho ya watu wale yalipofuka; hata hivyo si wao wenyewe wala wenzao wa kaumu hiyo walionasihika na kupata ibra kutokana na adhabu hiyo ya waziwazi ya Mwenyezi Mungu. Na sio tu watu hao hawakujutia waliyoyafanya, bali walidhamiria hata kumuua pia Nabii Lut AS. Na hapo ndipo Allah akamuokoa Mtume wake na watu wake wakati wa usiku na asubuhi yake akaiangamiza kaumu ya watu hao waovu na mafasiki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mwenyezi Mungu SWT huwa kwanza anatimiza dhima kwa watu kupitia Mitume wake na baadaye ndipo huwateremshia adhabu wapinzani na wakadhabishaji wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, inapofika hadi ya maasi na maovu kuzoeleka na kuonekana jambo la kawaida katika jamii, nyumba za waja safi, wema na waumini, nazo pia hazitasalimika na hujuma za watu wachafu na mafasiki. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Qur'ani si kitabu cha historia, lakini kinasimulia habari na hatima zilizowapata watu wa kaumu zilizopita, ili wale wanaokuja baada ya hao wapate ibra na mazingatio na iwe wepesi zaidi kwao wao kuikubali haki.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 41 na 42 ya sura yetu ya Al-Qamar ambazo zinasema:

وَلَقَدْ جَاءَ آلَ فِرْعَوْنَ النُّذُرُ

Na Waonyaji waliwafikia watu wa Firauni. 

كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كُلِّهَا فَأَخَذْنَاهُمْ أَخْذَ عَزِيزٍ مُّقْتَدِرٍ

Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika mshiko wa Mwenye nguvu, Mwenye uweza.

Kaumu ya tano ambayo hatima na mwisho mbaya ulioipata umezungumziwa ndani ya sura hii ya Al-Qamar ni kaumu ya Firauni, ambayo watu wake walikuwa wakimwabudu taghuti huyo kwa kumfanya kama mungu na kutii amri zake bila kuhoji wala kudadisi. Mafirauni walikuwa wakiwamiliki na kuwafanya watumwa watu wa kaumu ya Bani Israili na wakawa wanawatesa na kuwafanyia madhila na unyanyasaji wa kupindukia. Nabii Musa AS alimwendea kwanza Firauni kwa ajili ya kumlingania yeye na watu wa utawala wake wito wa Tauhidi wa kumwabudu Mola pekee wa haki na kwa ajili ya kuwakomboa pia Bani Israili kwa kuwatoa kwenye utumwa wa taghuti huyo. Kwa amri ya Allah, mtukufu huyo alimwonyesha Firauni na watu wake miujiza kadhaa, lakini badala ya kusilimu na kuikubali haki na kuacha ukafiri na dhulma wakadhamiria kumwangamiza Nabii Musa AS na wafuasi wake. Kwa sababu hiyo, Allah SWT aliwaangamiza madhalimu hao wote kwa kuwagharikisha kwenye maji ya Mto Nile. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwatii watawala madhalimu na mataghuti pamoja na kufuata fikra zao, kunamshirikisha mtu kwenye hatima na mwisho wao wa hapa duniani na huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, miujiza ya Mwenyezi Mungu inaletwa kwa ajili ya kuwaelewesha watu haki na kutimiza dhima juu yao, lakini watu wanaoiona miujiza hiyo kwa macho yao kisha wakaikadhibisha, hufikwa na adhabu hata hapa duniani pia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, nguvu na uwezo usioshindika ni wa Allah Jalla Jalalu peke yake; lakini nguvu na uwezo wa mwanadamu mbele ya uwezo mutlaki wa Mola si lolote si chochote, hata kama mwanadamu huyo ataonekana kidhahiri ni mwenye nguvu na uwezo mkubwa sana. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 972 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/  

 

 

Tags