Jeshi la IRGC latangaza utiifu kwa Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137246-jeshi_la_irgc_latangaza_utiifu_kwa_kiongozi_mpya_wa_mapinduzi_ya_kiislamu
Kufuatia kuchaguliwa kwa Ayatullah Seyed Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema liko tayari kikamilifu kutekeleza amri zake.
(last modified 2026-03-09T07:04:00+00:00 )
Mar 09, 2026 07:04 UTC
  • Jeshi la IRGC latangaza utiifu kwa Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kufuatia kuchaguliwa kwa Ayatullah Seyed Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema liko tayari kikamilifu kutekeleza amri zake.

Katika taarifa iliyotolewa mapema Jumatatu, IRGC ilisisitiza uungaji mkono wake kwa uamuzi wa Baraza la  Wanazuoni Wataalamu wa kumchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi.

Taarifa hiyo ilieleza uchaguzi huo kuwa ni kama kuchomoza kwa alfajiri mpya na kuanza kwa hatua mpya katika Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Iliongeza kuwa IRGC iko tayari kikamilifu kutii maelekezo ya Kiongozi mpya na kujitoa mhanga katika njia yake, huku ikiendelea na juhudi za kulinda na kuhifadhi maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu na kulinda urithi adhimu wa viongozi wawili waliotangulia wa Mapinduzi hayo, Imam Khomeini na Shahidi Ayatullah Imam Sayyid Ali Khamenei.

IRGC pia imewaalika wananchi wote na wale wanaoipenda Iran kuunga mkono mfumo wa Wilayat al‑Faqih (uongozi wa mwanazuoni wa sheria za Kiislamu).

Baraza la Wanazuoni Wataalamu nchini Iran limemchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi Muadhamu mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa Jumapili, tarehe 8 Machi 2026, Baraza hilo lilitoa rambirambi kufuatia kuuawa shahidi Imam Khamenei pamoja na mashahidi wengine waliouawa katika shambulizi la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 28 Februari. Aidha baraza hilo limelaani vikali kwa nguvu zote uvamizi huo wa kinyama wa Marekani mhalifu pamoja na utawala mwovu wa Kizayuni

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mara tu baada ya shahada ya Imam Khamenei, licha ya kuwepo kwa hali ya vita na vitisho vya moja kwa moja kutoka kwa maadui, Baraza la Wanazuoni Wataalamu halikupoteza muda katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, bali lilianza mara moja mchakato wa kumchagua na kumtangaza Kiongozi mpya.

Marekani na utawala wa Israel walianzisha mashambulizi dhidi ya Iran kuanzia asubuhi ya Jumamosi, tarehe 28 Februari.

Kujibu uvamizi huo wa Marekani na Israel uliosababisha kuuawa shahidi Imam Khamenei, pamoja na makamanda kadhaa wakuu wa kijeshi na mamia ya raia wakiwemo wanawake na watoto, Iran ilianzisha Operesheni Ahadi ya Kweli 4 , ikitekeleza mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya malengo ya Israel na vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Asia Magharibi.