Ayatullah Mojtaba Khamenei ni nani?
Miongoni mwa maswali muhimu yanayoulizwa sana wakati huu kuhusu Iran ni kwamba, Ayatullah Mojtaba Husseini Khamenei ni nani? Na kwa nini Baraza la Wataalamu limemchagua kuongoza Iran? Ili kuelewa chaguo hili, lazima kwanza tuangalie utaratibu wa kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, kiongozi wa nchi huchaguliwa na Baraza la Wataalamu, yaani kundi linalojumuisha wanasheria na wasomi wa kidini, ambalo wanachama wake huchaguliwa moja kwa moja na watu wa Iran.
Hii ina maana kwamba, wananchi kwanza huchagua wataalamu hao, na wao ndio wanaowajibika kuainisha Kiongozi Mkuu wa nchi.
Kwa hivyo, wakati Baraza la Wataalamu linapomchagua mtu kuwa Kiongozi Mkuu, uteuzi huo lazima uzingatie seti ya vigezo vya kisayansi, uwezo wa uongozi, na masuala ya kimkakati.
Katika kadhia ya Ayatullah Mojtaba Husseini Khamenei, mambo kadhaa muhimu yametajwa katika uamuzi huu.
Kwanza, historia yake ya kielimu na katika vyuo vikuu vya kidini.
Alisoma kwa miaka mingi katika hauza yaani vyuo vikuu vya kidini vya Qum na amepata elimu katika utamaduni wa kitaaluma na kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu; mazingira ambayo viongozi wengi na wanazuoni wa juu kabisa wa dini wanafunzwa na kunolewa.
Pili, ni uelewa wake wa kina wa muundo wa mfumo tawala.
Katika miongo kadhaa iliyopita, amekuwa akijifunza kwa karibu michakato ya kufanya maamuzi katika Jamhuri ya Kiislamu na anaelewa mifumo tata ya kisiasa na kiusalama ya nchi hii.
Tatu, ni uhusiano na ujuzi wake wa kina kuhusu taasisi muhimu za nchi.
Uzoefu na ujuzi wake kuhusiana na asasi muhimu za nchi kama vile Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na taasisi zingine za kimkakati umempa uelewa sahihi kuhusu usalama wa Iran na hali halisi ya kikanda.
Na nne, ni hali maalumu ya wakati huu.
Leo, Iran iko katika mazingira yenye mivutano na magumu sana.
Kuanzia vikwazo vya pande zote na mashinikizo ya kiuchumi hadi ushindani wa kikanda na vita mseto vya vyombo vya habari na usalama.
Katika mazingira kama hayo, wengi wanaamini nchi inahitaji kiongozi ambaye anatambua urithi wa kifikra wa Mapinduzi ya Kiislamu na anaelewa vyema changamoto mpya za dunia ya leo.
Kwa sababu hii, kwa maoni ya baadhi ya wachambuzi, hatua ya Baraza la Wataalamu ya kumchagua Ayatullah Mojtaba Khamenei ina maana ya mwendelezo wa njia ya kimkakati ya sera ya ndani na nje ya Iran; njia inayosisitiza kulindwa uhuru na mamlaka ya kujitawa ya nchi na kupinga mashinikizo ya kigeni.
Mwishowe, kilicho muhimu ni kwamba uchaguzi huu umefanywa ndani ya mfumo wa utaratibu uleule wa kisheria wa Jamhuri ya Kiislamu; yaani, kupitia taasisi ambayo wanachama wake huchaguliwa moja kwa moja na wananchi wa Iran.
Na jambo hili ndilo linaloupa uamuzi huu uhalali wa kisheria na kimuundo.