Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei achaguliwa kuwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu
-
Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei
Baraza la Wanazuoni Wataalamu nchini Iran limemchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi Muadhamu mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa Jumapili, tarehe 8 Machi 2026, Baraza hilo lilitoa rambirambi kufuatia kuuawa shahidi Imam Khamenei pamoja na mashahidi wengine waliouawa katika shambulizi la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 28 Februari. Aidha baraza hilo limelaani vikali kwa nguvu zote uvamizi huo wa kinyama wa Marekani mhalifu pamoja na utawala mwovu wa Kizayuni
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mara tu baada ya shahada ya Imam Khamenei, licha ya kuwepo kwa hali ya vita na vitisho vya moja kwa moja kutoka kwa maadui, Baraza la Wanazuoni Wataalamu halikupoteza muda katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, bali lilianza mara moja mchakato wa kumchagua na kumtangaza Kiongozi mpya.
Iliongeza kuwa baada ya uchunguzi makini na tathmini pana, na kwa kuzingatia wajibu wake wa kidini, Baraza hilo katika kikao chake cha Jumapili lilimchagua na kumtangaza Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel walianzisha mashambulizi dhidi ya Iran kuanzia asubuhi ya Jumamosi, tarehe 28 Februari.
Kwa kujibu uchokozi huo wa Marekani na Israel uliosababisha shahada ya Imam Sayyid Ali Khamenei, pamoja na makamanda kadhaa waandamizi wa kijeshi na mamia ya raia, wakiwemo watoto, Iran ilianzisha Operesheni Ahadi ya Kweli 4, ikitekeleza mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya malengo ya Israel na kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.