Sep 02, 2023 02:41 UTC
  • Jumamosi, Pili Septemba, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria mwafaka na tarehe Pili Septemba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita, baada ya vita kadhaa baina ya vikosi vya utawala wa Othmania na jeshi la Uingereza kwa upande mmoja na vikosi vya Ufaransa kwa upande mwingine, hatimaye Wafaransa walishindwa katika vita na kulazimika kuondoka kikamilifu nchini Misri. Ikumbukwe kuwa, baada ya Napoleone Bonaparte kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri, Uingereza ambayo katika zama hizo ilikuwa ikihesabiwa kuwa hasimu na mshindani mkuu wa Ufaransa katika masuala ya kiuchumi na kijeshi, ilihisi maslahi yake yakiwa hatarini. Ni kwa sababgu hiyo, ndio maana Uingereza ikaungana na utawala wa Othmania kwa shabaha ya kwenda kuitoa Ufaransa huko Misri na kuzuia jeshi la Ufaransa lisisonge mbele. ***

Bendera ya Syria

 

 Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu mahiri wa elimu ya fizikia wa Ireland alifariki dunia. Alizaliwa mwaka 1805 na kuonyesha kuwa mwerevu na mwenye kipaji cha hali ya juu tangu akiwa mtoto mdogo. Hamilton alisoma kwa ami yake aliyekuwa kasisi. Alipofikisha umri wa miaka 13, mwanafizikia huyo mtajika wa Ireland alikuwa tayari anazifahamu lugha kadhaa za kimataifa. Hadi anafikisha umri wa miaka 22 alikuwa tayari ni mwalimu katika elimu ya nujumu. ***

William Rowan Hamilton

 

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, nchi ya Vietnam ilipata uhuru. Vietnam ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katikati mwa karne ya 19. Mwaka 1940 nchi hiyo ikadhibitiwa na Japan baada ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Vietnam iliendelea kuwa chini ya utawala na udhibiti wa Japan hadi pale Japan iliposalimu amri mwishoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. ***

Bendera ya Vietnam

 

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, yaani tarehe Pili Septemba mwaka 1945, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilifikia tamati baada ya Japan kusalimu amri bila ya masharti yoyote. Baada ya Japan kushindwa mfululizo na majeshi ya waitifaki, ililazimika kusalimu amri katika vita hivyo, hasa baada ya miji yake miwili mashuhuri ya Hiroshima na Nagasaki kushambuliwa na Marekani kwa mabomu ya atomiki. Baada ya tukio hilo lililotokea miezi minne tu baada ya kusalimu amri Ujerumani, nchi waitifaki ziliikalia kwa mabavu Japan kwa mujibu wa Mkataba wa Potsdam na Generali wa Kimarekani, Douglas MacArthur, akachaguliwa kuwa kamanda mkuu huko Japan. Mwaka 1951, nchi 49 duniani zilitiliana saini mkataba wa amani na Japan, na mwaka mmoja baadaye nchi hiyo kwa mara nyingine tena ikaanza kujitawala na kujiamulia mambo yake yenyewe. ***

Kusalimu amri Japan na hivyo kufikia tamati Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

 

Tarehe 11 Shahivar miaka 61 iliyopita mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 7.3 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika eneo la Buin Zahra huko kaskazini magharibi mwa Iran. Mtetemeko huo mkubwa uliua zaidi ya watu elfu 20 na kujeruhi maelfu ya wengine. Mtetemeko huo wa ardhi ulitokea nyakati za usiku na hivyo haukuwapa watu fursa ya kuokoa maisha yao. Mtetemeko huo wa Buin Zahra uliharibu kabisa vijiji 120 na kusababisha hasara kubwa katika mamia ya nyumba za eneo hilo. Baada tu ya mtetemeko huo wananchi wa Iran waliharakia kuwapelekea misaada wenzao wa Buin Zahra. ***

Mtetemeko wa ardhi ulitokea katika eneo la Buin Zahra kaskazini magharibi mwa Iran