Jumatatu, Oktoba 12, 2026
Leo ni Jumatatu mwezi Mosi Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1448 Hijria ambayo inasadifiana na 12 Oktoba 2026 Miladia.
Leo tarehe 20 mwezi wa Mehr kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia, inasadifiana na maadhimisho ya kumuenzi Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, mshairi na malenga mkubwa wa Kiirani. Hafiz alizaliwa mwaka 727 Hijiria Shamsia huko Shiraz moja kati ya miji ya kusini mwa Iran. Alikuwa mtaalamu wa tafsiri ya Qur'ani, falsafa na fasihi ya Kiarabu na alipata umashuhuri kwa jina la Hafiz kutokana na kuhifadhi kwake Qur'ani Tukufu kwa visomo tofauti. Mbali na elimu hizo, Khaja Shamsuddin Muhammad Hafiz Shirazi, alikuwa mtaalamu mkubwa wa elimu ya Irfan.
***
Siku kama ya leo miaka 237 iliyopita yaani tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1211, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la "Al Uzriya" ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000.
***
Katika siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, yaani tarehe 20 Mehri 1192 Hijria Shamsia kulitiwa saini mkataba wa aibu wa "Golestan" kati ya Iran na Russia. Mkataba huo ulitiwa saini kufuatia kushindwa Iran na Russia. Mkataba huu ulitiwa saini baada ya kumalizika kwa duru ya kwanza ya vita vya Iran na Russia, ambavyo vilidumu kwa miaka kumi na ulitiwa saini kwa uingiliaji kati wa serikali ya Uingereza. Kulingana na makubaliano haya, miji yote ambayo ilikuwa imechukuliwa na Russia hadi wakati huo ilibaki kuwa sehemu ya Russia, na umiliki wa Russia kwa miji ya Karabakh, Baku, Darband, Lankaran, na sehemu ya Talesh pia ulikubaliwa.
***
Katika siku kama ya leo miaka 139 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Husseini Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu. Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni.
***
Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Anatole France, mwandishi wa riwaya, mwanafasihi na mwanafalsafa wa Ufaransa. Anatole France, alizaliwa katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris. Baba yyake alikuwa muuza vitabu na sehemu kubwa ya maisha ya Anatole France ilitawaliwa na vitabu. Mwaka 1921 mwandishi huyo mahiri wa Kifaransa alitunukiwa tuzo ya Nobel katika uga wa fasihi.
***
Tarehe 12 Oktoba miaka 27 iliyopita, Jenerali Parviz Musharraf, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Pakistan alifanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo Muhammad Nawaz Sharrif. Baada ya mapinduzi hayo Musharraf ambaye alichukua madaraka ya rais wa nchi, alivifanyia mabadiliko baadhi ya vipengee vya katiba ya nchi hiyo na kuzidisha nguvu na uwezo wa rais. Hata hivyo kutokana na kuongezeka mashinikizo ya ndani na nje, Musharraf alisalimu amri mwezi Novemba 2007 na kuachia cheo cha Mkuu wa majeshi ya Pakistan. Musharraf aliondoka kikamilifu madarakani mwezi Julai 2008, baada ya kushika kasi vyama vya upinzani ambavyo vilishinda uchaguzi wa rais.
***
Tarehe 12 Oktoba ni Siku ya Taifa nchini Uhispania. Nchi ya Uhispania, yenye eneo la takribani kilomita za mraba 504,782, iko kusini-magharibi mwa Ulaya, ikipakana na Bahari ya Atlantiki na Bahari ya Mediterania. Inapakana pia na nchi za Ureno, Andorra na Ufaransa. Tangu zamani sana, Hispania imekuwa makazi ya watu na makabila mbalimbali. Kabla ya kuzaliwa Kristo, Wafoinike na Wakarthage waliishi katika eneo hilo. Baadaye Hispania ikawa sehemu ya Dola ya Roma. Katika karne ya 7 BK, majeshi ya Kiislamu yaliingia Hispania, na kuanzia wakati huo ukaanza ujumbe/kipindi cha Kiislamu katika historia ya Hispania. Enzi mpya ya Hispania ilianza mwaka 1492, baada ya Christopher Columbus (Kristoforo Kolumbus) kugundua Amerika. Katika karne zilizofuata, Hispania iligeuka kuwa dola kubwa na yenye nguvu, ikiwa na makoloni katika sehemu mbalimbali za dunia. Katika karne ya 19, himaya hiyo ilianza kudhoofika. Utawala wa kifalme uliendelea nchini humo hadi baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Mwaka 1931, Warepublican walishinda na Hispania ikawa jamhuri. Katika miongo mitatu ya katikati ya karne ya 20, Hispania ilitawaliwa kidikteta na Jenerali Francisco Franco. Kwa sasa, mfumo wa serikali ya Hispania ni ufalme wa kikatiba wenye mabunge mawili. Tarehe 12 Oktoba 1492, ambayo inahusishwa na safari ya Christopher Columbus na ugunduzi wa Amerika, ndiyo iliyochaguliwa kuwa Siku ya Kitaifa ya Hispania.
***