Araghchi: Wavamizi hawapaswi kukwepa kuwajibika kwa jinai walizotenda
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, haipaswi kuruhusiwa wavamizi kukwepa kuwajibika kwa vitendo vyao vya uhalifu na jinai walizotenda.
Sayyid Abbas Araghchi amesisitiza kuwa mazingira ni turathi ya pamoja ya binadamu, na hayapaswi kugeuzwa kuwa uwanja wa mashindano, nyenzo ya kuweka shinikizo la kisiasa, wala kuathiriwa na maslahi ya muda mfupi ya kiuchumi na kijeshi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema kuwa, mazingira hayawezi tena kuchukuliwa kama mhanga wa kimya wa vita.
Akizungumza Jumapili ya jana (11 Oktoba) katika kongamano la kimataifa lililopewa jina la “Ecocide: Uhalifu wa Kivita wa Kimya,” Araghchi amesema kuwa, vita na migogoro ya kivita havilengi tu maisha ya binadamu, miji na miundombinu ya kiuchumi na kijamii, bali pia husababisha madhara makubwa kwa mazingira.
Ameeleza kuwa, maji, udongo, hewa, misitu, mashamba, vyanzo vya nishati, makazi ya viumbe wa asili na bioanuwai (anuwai ya viumbe hai) vyote hukabiliwa na athari za uharibifu unaosababishwa na vita.
Araghchi ameeleza kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, huko Gaza, Lebanon na Iran, imeshuhudiwa jinsi mashambulizi ya kijeshi, mbali na kusababisha vifo vya watu na uharibifu wa miundombinu muhimu, yalivyoacha madhara makubwa na wakati mwingine ya kudumu kwa mazingira.
Amesisitiza kuwa, kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sheria za kimataifa hazipaswi kubaki kimya mbele ya uharibifu wa mazingira na ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu wakati wa vita.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, utekelezaji madhubuti wa kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu, zikiwemo kanuni ya kutofautisha raia na wapiganaji pamoja na kanuni ya uwiano wa nguvu zinazotumika, unapaswa kupewa kipaumbele. Aidha, ni muhimu kuzingatia kwa uzito madhara ya moja kwa moja, yasiyo ya moja kwa moja na ya muda mrefu ambayo operesheni za kijeshi husababisha kwa mazingira.
Araghchi ameongeza kuwa, sheria za kimataifa za kibinadamu, zikiwemo kanuni zinazolinda mazingira ya asili wakati wa migogoro ya kivita, lazima ziheshimiwe kikamilifu. Ameonya kuwa jamii ya kimataifa haiwezi kubaki bila kujali madhara ya kimazingira yanayotokana na vita.