Sep 14, 2023 02:25 UTC
  • Alkhamisi, Septemba 14, 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Mfunguo Tano Safar 1445 Hijria, mwafaka na tarehe 14 Septemba 2023 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63.

Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga.

Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake. 

Siku kama ya leo miaka 1395 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw).

Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo aliweza kunufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kufariki dunia Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama pamoja na ukwamishaji mambo wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah. Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufyan.

Katika siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, moja kati ya ajali kubwa za moto ulimwenguni ilitokea katika mji mkuu wa Russia Moscow. Moto huo uliwashwa kwa makusudi. Ilikuwa imepita siku moja tu, tangu mji huo uvamiwe na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte, wakati mji huo ulipochomwa moto kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa mji huo. Lengo la mtawala huyo lilikuwa kuyafanya majeshi ya Bonaparte yashindwe kutumia suhula za mji huo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji wa Moscow.

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita yaani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake. Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behest Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao. Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huku wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini na kiongozi wetu.”

 

Tags