Oct 03, 2023 23:05 UTC
  • Jumatano tarehe 4 Oktoba 2023

Leo ni Jumatano tarehe 18 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1445 Hjria sawa na Oktoba 4 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1444 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, ilianza kazi ya ujenzi wa Msikiti wa Mtume mjini Madina ambao ni msikiti wa pili kwa utukufu duniani baada ya Masjidul Haram. Mtume (SAW) alitoa amri ya kujengwa msikiti wa Madina baada tu ya kuhamia mjini humo na yeye mwenyewe alishiriki katika ujenzi wake. Kandokando ya msikiti huo kulijengwa vyumba vya Mtume na baadhi ya maswahaba zake. Mtume hakuutumia msikiti kwa ajili ya ibada tu, bali alitumia pia sehemu hiyo kwa ajili ya masuala kama kutoa hukumu baina ya watu, vikao vya mashauriano, mafunzo ya kivita na utatuzi wa masuala mbalimbali ya Waislamu.

Masjidu Nabi

Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo. 

Bendera ya Ubelgiji

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasi wasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda. 

Alexander Fleming

Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini. 

Na siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Serikali ya Kuwait ilimnyima Imam Khomeini ruhusa ya kuishi nchini humo na hivyo akulazimika kuelekea nchini Ufaransa. Hatua ya Imam kuelekea Paris, ilikuwa sababu ya kuharakisha mwenendo wa mafanikio ya Mapinduzi nchini Iran, kinyume kabisa na matarajio ya dikteta Saddam wa Iraq na Mohammad Reza Pahlavi, mfalme kibaraka wa wakati huo wa Iran ambao waliamini kwamba, kwa kumbaidisha Imam Khomeini (MA) wangekuwa wameua harakati zake za kimapinduzi. Akiwa mjini Paris, Imam aliishi katika kijiji kilichoitwa Neauphle-le-Château, kilometa 50 kutoka mji huo, ambapo aliendeleza harakati zake za kimapinduzi kupitia barua na kanda za sauti kwa wanamapinduzi nchini Iran. 

Imam akiondoka Iraq