Oct 06, 2023 22:56 UTC
  • Jumamosi 7 Oktoba, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 21 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe 7 Oktoba 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita mji wa Yerevan ulioangukia mikononi mwa vikosi vya Russia wakati wa kujiri vita vya pili kati ya Iran na Russia. Mji huo ulitekwa katika zama za utawala wa Fat'h Ali Shah Qajar na ukakabidhiwa kwa Warusi. Natija ya kushindwa huko kukawa ni kusainiwa mkataba wa Turkmenchay (Treaty of Turkmenchay). Kwa mujibu wa mkataba huo na kutokana na kutokuwa na ustahiki Shah Qajar sehemu kubwa ya ardhi ya kaskazini mwa Azerbaijan na Caucasia ilitengwa na ardhi ya Iran na kuunganishwa na Russia. ***

Mkataba wa Turkmenchay (Treaty of Turkmenchay)

 

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kufuatia kushadidi harakati za kupigania katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kufanikisha kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alazimika kutekeleza jambo hilo. ***

 

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan. ***

Sohrab Sepehri

 

Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti lilivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo. ***

Ujerumani

 

Miaka 30 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, mwanazuoni wa fakihi Ayatullah Hassan Muhammadi Laini aliaga dunia. Alizaliwa katika moja ya vijiji vya Busheh Iran. Laini alimpoteza baba yake aliyeaga dunia wakati yeye akiwa angali mdogo na kulelewa na mama yake. Baada ya masomo ya msingi alielekea Najaf Iraq na kubakia huko kwa muda wa miaka 12 akihudhuria darsa na masomo ya wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Sayyid Mahmoud Shahroudi na Mirza Hashhim Amoli. Ayatullah Hassan Muhammadi Laini alishiriki pia katika harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Kipahlavi na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kkiislamu alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Mazandaran kwa duru mbili katika Baraza la Wanazuoni la Kumchagua Kiongozi Muadhamu na kusimamia kazi zake. ***

Ayatullah Hassan Muhammadi Laini

 

Miaka 22 liyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.  ***

Hujuma na uvamizi wa Marekani nchini Afghanistan