Jumapili 8 Oktoba, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 22 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1445 Hijria mwafaka na tarehe 8 Oktoba 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (saw).
Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakutakiwa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla.
Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao. ***
Miaka 142 iliyopita katika siku kama ya leo, kimbunga kikubwa kilitokea nchini Vietnam. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na tufani hiyo kubwa yalikuwa ya kusini mwa nchi hiyo. Kimbunga hicho kiliharibu mashamba na kubomoa kikamilifu nyumba za maeneo ya kusini mwa Vietnam. Aidha kufuatia janga hilo la kimaumbile, zaidi ya watu 300,000 waliaga dunia. ***

Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, vita vya Balkan vilianza kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya Utawala wa Othmania.
Ufalme wa Othmania kwa miaka kadhaa mtawalia ulikuwa umefanikiwa kuyafanya maeneo mengi ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya kuwa chini ya udhibiti wake na hivyo ukawa umetanua utawala wake.
Vuguvugu la kulitaka kujitenga nchi zilizokuwa chini ya utawala huo lilikuwa likipelekea kutokea vurugu mara kwa mara na vita vya Balkan ni moja ya harakati hizo. ***
Miaka 95 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 16 Mehr mwaka 1307 Hijiria Shamsia kufuatia upinzani wa Sayyid Hassan Mudarres dhidi ya udikteta wa Reza Khan Pahlawi, mtawala huyo aliwaamuru askari wake wavamie nyumba ya Ayatullah Muddares, kumpiga na kumjeruhi na kisha akahamishiwa nje ya mji wa Tehran.
Askari hao pia waliwatia nguvuni watu wa familia ya mwanazuoni huyo. Mwishowe Ayatullah Mudarres alibaidishwa katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran na kuuawa shahidi na askari wa Reza Khan mwaka 1316 Hijiria Shamsia. ***
Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, utawala wa Baath wa Iraq uliushambulia kwa mabomu ya kemikali mji wa Sumar wa Iran.
Raia wengi waliuawa shahidi katika shambulio hilo. Katika kkipindi cha miaka 8 ya vita vya kichokozi ilivyoansisha dhidi ya Iran, utawala wa Saddam ulitumia mara kkadhhaa silaha za kemikali. Takribani raia laki moja waliuawa shahidi au kujeruhiwa katika tukio hilo la kinyama. ***
Na miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo, mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha Rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan.
Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu wapatao 90 elfu walipoteza maisha yao na wengine milioni 3 na laki 6 kubaki bila makazi kufuatia mtetemeko huo. ***